MERSEYSIDE, Uingereza
AKIWA Liverpool, Trent Alexander-Arnold, aliweza kufika daraja la juu la soka, akitajwa kuwa miongoni mwa mabeki wa kulia bora kuwahi kutokea katika historia ya Ligi Kuu ya England [EPL].
Upepo ulibadilika ghafla alipoondoka Anfield na kutimkia La Liga kujiunga na Real Madrid. Alicheza mechi 30 pekee katika msimu wake wa kwanza Hispania, hiyo ikitokana na wimbi la majeraha.
Na sasa, licha ya Madrid kuwa chini ya kocha mpya, Jose Mourinho ‘Special One’, bado Alexander Arnold hana uhakika wa kuingia kikosi cha kwanza pale Santiago Bernabeu.
Kushindwa kwake kucheza mara kwa mara katika kikosi cha Madrid kumemfanya nyota huyo kupoteza kabisa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya Taifa ya England.
Ian Rush
Mfungaji bora wa muda wote wa Liverpool. Katika kilele cha ubora wake, Rush aliondoka na kujiunga na Juventus, ambako hata hivyo mambo hayakuwa mazuri kwa upande wake.
Alikwenda Juventus akiwa mfungaji bora wa Liverpool lakini aliishia kufunga mara saba pekee.
Michael Owen
Akiwa ametwaa tuzo ya Ballon d’Or akiwa Liverpool, Owen aliondoka na kutimkia Real Madrid alikokutana na mastaa wengi, wakiwamo Kaka, Ronaldo Nazario na Zinedine Zidane.
Maisha yake katika klabu ya Madrid yaliandamwa na majeraha mengi, kiasi cha kupoteza kabisa ubora aliotoka nao Anfield.
Philippe Coutinho
Baada ya Barcelona kuona staa wake, Neymar, ametimkia PSG kwa ada ya euro milioni 222, mabosi wa klabu hiyo ya Hispania waliamua kuibomoa Liverpool kwa kumsajili Mbrazil mwenzake, Coutinho.
Mambo hayakwenda vizuri kwa Coutinho akiwa Barcelona, ingawa Liverpool wao walinufaika zaidi kwani sehemu ya fedha walizopata walitumia kuwasajili Virgil van Dijk na Alisson.
Georginio Wijnaldum
Alifanya kazi kubwa kwenye eneo la kiungo wakati Liverpool inatwaa mataji ya Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu lakini staa huyo wa kimataifa wa Uholanzi aliamua kuondoka mwaka 2021.
Licha ya kupokea ofa ya Barcelona iliyokuwa chini ya Ronald Koeman, Wijnaldum aliamua kutimkia PSG. Hakuweza kuwika, kisha akatolewa kwa mkopo kwenda AS Roma ya Serie A.
Sadio Mane
Akishirikiana na Mohamed Salah na Firmino, Mane aliweza kuwa mmoja ya washambuliaji wa daraja la juu barani Ulaya.
Mambo yalibadilika ghafla baada ya uamuzi wake wa kuondoka Liverpool na kujiunga na Bayern Munich. Alicheza kwa muda mfupi tu, kisha akaondoka zake na kwenda Saudi Arabia.
Fernando Torres
Baada ya kufunga mabao 81 katika mechi 142, mshambuliaji huyo raia wa Hispania aliondoka Liverpool na kujiunga na Chelsea.
Akiwa Stamford Bridge, upepo ukabadilika, ambapo alifunga mabao 45 pekee katika mechi 172, huku akiandamwa na wimbi la majeraha. Baadaye, alitimkia AC Milan, kisha Atletico Madrid, Sagan Tosu ya Japan, kabla ya kustaafu mwaka 2019.


