Na mwandishi wetu, Gazetini-Morogoro
WAJUMBE wa Bodi za Zabuni kutoka taasisi nunuzi nchini wametakiwa kuzingatia uadilifu, uzalendo na weledi katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha manunuzi ya umma yanasimamiwa kwa mujibu wa sheria, kulinda rasilimali za Taifa na kutanguliza maslahi ya umma.
Akifungua mafunzo hayo jijini Morogoro leo Jumanne, Novemba 24, 2026, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dk. Mussa Ali Mussa, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu, Sebastian Masanja, amesema matumizi sahihi ya mfumo wa NeST yanapaswa kwenda sambamba na misingi ya maadili.

Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia pekee hayawezi kuleta matokeo yanayotarajiwa bila kuwepo kwa uadilifu miongoni mwa watendaji wanaohusika na michakato ya ununuzi.
Aidha, amewataka washiriki kutumia maarifa watakayoyapata katika mafunzo hayo kuboresha utendaji wa taasisi zao na kuhakikisha michakato ya ununuzi inatekelezwa kwa wakati, kwa ubora unaostahili na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha za umma.

Awali, Mkurugenzi wa Utafiti, Maendeleo na Ubunifu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Mhandisi Masunya Eliakim Nashon, amesema mamlaka hiyo inalenga kuhakikisha washiriki wanafahamu matakwa ya Serikali katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Kuendeleza Uwezo na Huduma za Ushauri wa PPRA, Gilbert Kamnde, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za mamlaka hiyo kuhakikisha watumiaji wa mfumo wa NeST pamoja na wadau wanaojihusisha na masuala ya ununuzi na ugavi wanapata elimu sahihi itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Naye, miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, Benedict Bugambi na Lenatha Miruko, wamesema mafunzo hayo yatawaongezea ujuzi na kuwasaidia kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na PPRA yanalenga kuimarisha uwezo wa wajumbe wa Bodi za Zabuni katika matumizi ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na mfumo wa NeST, hususan moduli ya Bodi za Zabuni, kwa lengo la kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika manunuzi ya umma nchini.Bodi za zabuni zatakiwa kuzingatia uadilifu katika manunuzi ya umma


