RIO, Brazil
MWAKA 2026 unakwenda kumalizika ukiwa umeacha maumivu makali kwa binadamu mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za nchini Brazil, Flavio Bolsonaro.
Baada ya skendo nyingi zilizochafua taswira ya familia yake mbele ya raia wa nchi hiyo, Bolsonaro amepoteza kiti cha urais kupitia Uchaguzi Mkuu uliofanyika miezi michache iliyopita.
Muda mfupi tu baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo yaliyompa ushindi Luiz Inacio Lula da Silva aliyekusanya kura zaidi ya milioni nne, Bolsonaro aliongozana na familia yake wakitumia ndege binafsi kutimkia Marekani.
Saa chache baada ya kutua huko, Bolsonaro alituma salamu nyumbani kwa kuishambulia kwa maneno Mahakama Kuu aliyodai kuwa ilimpora ushindi aliostahili, akifananisha ushindi wa Lula da Silva na mapinduzi ya kijeshi.
FAMILIA YA UFISADI
Bolsonaro ambaye amekuwa akiungwa mkono na Serikali ya Marekani chini ya Rais Donald Trump, ameondoka Brazil akiwa anakabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha na rushwa.
Moja ya shutuma zinazomkabili ni kupokea fedha kinyume cha sheria kutoka kwa mtandao wa Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance.
Kwa upande mwingine, Bolsonaro ni kama anapitia njia za baba yake, Jair Bolsonaro, ambaye pia aliwahi kuwa Rais wa Brazil, kisha kukimbilia Marekani mwaka 2022 baada ya kuangushwa na Lula da Silva.
Mwaka 2025, kaka yake, Eduardo, naye alikimbilia uhamishoni nchini Marekani baada ya taarifa kuvuja kuwa aliendesha kampeni ya kimyakimya kutaka nchi yake iwekewe vikwazo.
Kwa wachambuzi wa siasa, tabia hii ya familia hiyo kukimbilia kwa Rais Trump kila inapokabiliwa na shutuma kumeishushia heshima kubwa iliyowahi kuwa nayo hapo awali.
Aidha, hiyo imemfanya Rais wa sasa, Lula, kuonekana shujaa zaidi kwani hakukimbia nchi, na badala yake alikubali kusota gerezani wakati akikabiliwa na mashitaka mbalimbali, yakiwamo ya rushwa.
MKAKATI WA KUING’OA SERIKALI?
Baadhi ya wachambuzi wanaliona hilo, kwamba Bolsonaro anaweza kushirikiana na Marekani kuunda uasi dhidi ya Serikali iliyoko madarakani nchini Brazil, wakitolea mfano kilichotokea Cuba na Venezuela.
Tofauti na Cuba na Venezuela, jumuhiya za kimataifa, zikiwamo zinazomuunga mkono Rais Trump, zimekwishakubali kuwa Lula ni rais halali wa Brazil.
Pia, tofauti na Cuba na Venezuela, diaspora wa Brazil waishio Marekani hawashawishiki na siasa, na badala yake wako nchini humo kujitafutia maisha mazuri waliyokosa nyumbani.
Hata hivyo, bado ‘mizizi’ ya familia ya Bolsonaro haijakwisha kabisa kwenye siasa za Brazil kwani mama yao, Michelle, ni Seneta mjini Brasilia, na ana ushawishi mkubwa kwa wanawake nchini humo.
Kama hiyo haijatosha, watoto watatu wa kiume, kwa maana ya Carlos, Renato na Renan, ni watumishi wa Serikali. Je, watapindua meza na kuirudishia utawala familia yao iliyopoteza mvuto kwa sasa?


