SEOUL, Korea ya Kusini
MWANAFUNZI aliyeongoza kwa matokeo mazuri ya mitihani ya ushauri wa kodi nchini Korea ya Kusini, Han Won-seok, amekiri kuwa hakutumia akili yake, bali aliwezeshwa na matumizi ya ‘akili-unde’ [AI].
Aidha, Won-seok amefichua alivyoingia kwenye chumba cha mtihani akiwa na kamera ndogo, simu na zana za teknolojia hiyo ya AI.
Won-seok ameanika ukweli huo kupitia video fupi aliyojirekodi na kuichapisha katika akaunti ya YouTube ya mwanasheria wake, Lee Don-Ho.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 34, aliongoza kwa matokeo mazuri baada ya kupata alama 397.5 kati ya 400 katika mitihani ya raundi ya kwanza.
Kwamba Won-seok alikosa swali moja tu kati ya 160, jambo lililozua mjadala mkubwa wa namna alivyoweza kufaulu kwa kiwango kikubwa kiasi hicho.
“Niliibia katika raundi ya kwanza na ya pili ya mitihani ya ushauri wa kodi kwa kutumia vifaa vya kielektroniki na AI,” amesema Won-seok katika video hiyo ya YouTube.
“Nilitumia kamera ndogo kupiga picha maswali na kuyatuma AI, kisha kuangalia majibu kupitia ‘simu-janja’ [smartphone].”
Tangu alipofaulu kwa kiwango cha kushitua, wengi walitilia shaka, ingawa Won-seok aliendelea ‘kukaza’ kwamba alitumia akili yake.


