9.2 C
New York

CRDB ‘yaliamsha dude’ mashindano ya baiskeli Shinyanga

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini – SHINYANGA

KATIKA juhudi za kuendeleza vipaji vya mchezo wa mashindano ya mbio za baiskeli, Benki ya CRDB imeandaa mashindano maalumu ya vijana wa ndani na nje ya Tanzania, huku washiriki wakiiomba Serikali kuweka mazingira rafiki ya mazoezi.

Katika mashindano hayo yaliyofanyika mkoani Shinyanga jana Novemba 14, 2026, Boniface Ngwata, mshiriki kutoka Dar es Salaam, aliibuka mshindi kwa upande wa wanaume, akishikiri umbali wa Kilometa 150 kwenda na kurudi kutoka Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, hadi Kijiji cha Mwakata, Kahama.

Licha ya kururahia ushindi huo, Mgwata amesema changamoto kubwa inayoukabili mchezo wa mbio za baiskeli nchini ni kukosekana kwa miundombinu rafiki, hivyo kupishana na magari barabarani, hasa wakati wa mazoezi.

“Usalama haupo, madereva hawatuheshimu hadi wanatutolea kauli chafu. Ikiwa tunahatarisha maisha yetu katika mchezo huu, tunaiomba Serikali ituangalie na sisi,” amesema Ngwata.

Naye mshindi wa nafasi ya kwanza upande wa wanawake kutoka Mkoa wa Dar-es-Salaam, aliyeshiriki umbali wa Kilometa 60 kutoka Uwanja wa Kambarage hadi Tinde na kurudi, Joline Juma, amesema bado wanawake ni wachache kwenye mchezo huo.

“Kikubwa kinachopelekea ushiriki wa wanawake kuwa mdogo, pengine ni uwoga. Nawasihi tu wasiogope na wajitokeze kwa wingi kushiriki mchezo huu,” amesema Joline na kuongeza kuwa idadi ya wanawake watano walioshiriki kwenye mashindano hayo inaonesha wazi kuwa kuna mwamko, licha ya jitihada kuhitajika zaidi.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, amesema mashindano hayo ni jukwaa la kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa uchangiaji damu, pamoja na umuhimu wa kutunza fedha katika akaunti za benki.

Aidha, Mgeni rasmi wa mashindano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema mikakati ya mwaka ujao ni kuyafanya mashindano hayo kuwa ya kimataifa kwa kushirikiana na wadau wengine wa michezo.

“Nitawasumbua sana CRDB. Tunataka mashindano yajayo yawe ya kimataifa na yaoneshwe ‘live’. Tutakaa kama kamati pamoja na wadau wa michezo na kujadili nini kifanyike ikibidi hata kushirikiana na Wizara husika ili kuyaongezea nguvu,” amesema Mtatiro.

Related articles

Recent articles