5 C
New York

Ngatunga; Mtanzania anayewapa samaki majina ya kisayansi

Published:

Na Faraja Mulungu, Gazetini-DAR

ANA shahada ya uzamivu katika taaluma ya utambuzi na uainishaji wa viumbe, amehusika kutoa majina ya kisayansi kwa aina 12 za samaki na kugundua aina mpya katika Ziwa Nyasa.

Katika utafiti wa viumbe wa majini, samaki hawatambuliki kwa majina yao ya kawaida pekee. Kila aina inahitaji kuwa na jina la kisayansi linalotambulika kimataifa ili kurahisisha utambuzi na mawasiliano miongoni mwa wanasayansi duniani.

Hata hivyo, kazi ya kutoa majina hayo si jambo rahisi. Inahitaji utaalamu wa kina, utafiti wa muda mrefu na uchunguzi wa tabia pamoja na maumbile ya samaki husika.

Benjamin Ngatunga, Mratibu wa Miradi wa Tanzania Tuna Fish National Alliance (Tuna Alliance).

Kwa Mtanzania Benjamin Ngatunga, ambaye ni Mratibu wa Miradi wa Tanzania Tuna Fish National Alliance (Tuna Alliance), hiyo ndiyo taaluma aliyoichagua na kujikita nayo hadi kufikia kiwango cha shahada ya uzamivu (PhD).

Akizungumza na Gazetini hivi karibuni kando ya warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa uhifadhi, wakiwamo waandishi wa habari, iliyofanyika mkoani Morogoro chini ya uratibu wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), Ngatunga anasema baada ya kusomea masuala mbalimbali ya uvuvi, alijikita katika taaluma ya taksonomia, inayohusika na utambuzi, uainishaji na utoaji wa majina ya kisayansi kwa viumbe.

Anabainisha kuwa majina ya kawaida ya samaki yanaweza kutofautiana kulingana na maeneo, lakini majina ya kisayansi yana kanuni zinazowezesha aina moja ya samaki kutambulika kwa jina moja duniani kote.

“Unakuta samaki yuleyule Tanga wanamwita jina jingine, Mtwara anaitwa jina jingine, lakini kisayansi anatakiwa kuwa na jina linalotambulika. Ndiyo maana nimejikita katika kuwapa majina samaki ambao hawajapewa majina rasmi,” anasema.

Anasema alivutiwa na taaluma hiyo kutokana na ugumu wake, hasa baada ya kukutana na kazi iliyokuwa imewashinda wataalamu wengine na kuamua kuifanyia utafiti hadi kuikamilisha.

Ametoa majina kwa samaki 12

Katika safari yake ya kitaaluma, Ngatunga anasema amehusika kutoa majina ya kisayansi kwa aina 12 za samaki, huku pia akigundua aina mpya ya samaki katika Ziwa Nyasa kupitia utafiti wake wa shahada ya uzamivu.

Anasema miongoni mwa samaki aliowafanyia utafiti ni wale wa jamii ya furu wanaopatikana Ziwa Nyasa, ambao walihitaji kuchunguzwa kwa kina, ikiwemo tabia zao za uzalianaji.

Samaki aina ya furu

Anaeleza kuwa utafiti huo ulihusisha kuchunguza namna samaki hao wanavyojenga viota chini ya maji, jinsi madume yanavyovutia majike na namna wanavyochagua wenza kabla ya kuzaliana.

Kwa mujibu wake, taarifa hizo ni muhimu katika kutofautisha aina za samaki, kwa kuwa utoaji wa jina la kisayansi hauishii kuangalia mwonekano wa nje pekee, bali unahitaji ushahidi wa kisayansi.

Ngatunga anasema Ziwa Nyasa lina aina takribani 800 za samaki ambazo tayari zinajulikana, lakini idadi hiyo inaweza kufikia 1,000 kutokana na uwezekano wa kuwepo kwa aina nyingine ambazo bado hazijagunduliwa.

Anasema hali hiyo inaonesha ukubwa wa kazi inayosubiri watafiti, si katika maziwa pekee bali pia katika maeneo ya kina kirefu baharini ambako viumbe wengi bado hawajafanyiwa utafiti wa kutosha.

Utafiti unaohitaji safari za kimataifa

Licha ya umuhimu wake, Ngatunga anasema taaluma hiyo ina changamoto kubwa, ikiwemo gharama na ugumu wa kupata vielelezo vya samaki vilivyotumika kwa mara ya kwanza kuelezea aina fulani ya samaki.

Anaeleza kuwa kabla ya kutoa jina jipya au kubadilisha jina lililokuwepo, mtafiti anapaswa kulinganisha samaki anayemchunguza na vielelezo vinavyohifadhiwa katika makumbusho ya kisayansi.

Kielelezo cha kwanza kilichotumika kuelezea aina fulani ya samaki huitwa holotype, na mtafiti anahitaji kufika mahali kilipohifadhiwa ili kukichunguza na kuthibitisha kama kinafanana na samaki anayemfanyia utafiti.

Anasema mara nyingi vielelezo hivyo huhifadhiwa katika makumbusho yaliyoko nje ya nchi, jambo linalomlazimu mtafiti kupata ufadhili wa safari na kufanya uchunguzi huo ana kwa ana.

“Ukiwa unafanya utafiti, lazima ujue samaki huyo alielezewa na nani, mwaka gani na kielelezo chake cha kwanza kimehifadhiwa katika makumbusho gani. Lazima ufike ukione ili uweze kufanya ulinganisho sahihi,” anafafanua.

Changamoto nyingine ni kushughulika na vielelezo vingi vilivyohifadhiwa kwa kutumia kemikali, ikiwemo formalini, jambo linalohitaji umakini na tahadhari wakati wa kuvichunguza.

Nafasi yake katika uhifadhi wa samaki

Mbali na taaluma yake ya utafiti wa samaki, Ngatunga ni Mratibu wa Miradi wa Tanzania Tuna Fish National Alliance, taasisi iliyosajiliwa nchini kama Asasi ya Kiraia (CSO), yenye wanachama 21 ambao ni taasisi na wadau wa sekta ya uvuvi.

Anasema Tuna Alliance ilianzishwa kwa msukumo wa Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), baada ya kuandaliwa kwa mpango wa usimamizi wa rasilimali za jodari. Uhitaji wa kuwa na taasisi itakayosaidia kusimamia utekelezaji wa mpango huo na kutetea uvunaji endelevu wa samaki hao ukachochea kuanzishwa kwake.

Anasema kwa sasa meli za uvuvi za kigeni ndizo zinazotumia zaidi rasilimali za jodari, huku wavuvi wadogo wa Tanzania wakikosa kunufaika kikamilifu kutokana na changamoto za kutumia mbinu na vifaa vinavyowezesha uvuvi huo kufanyika kwa ufanisi.

Sehemu ya Ziwa Nyasa.

Kwa maelezo yake, Tuna Alliance inalenga kuwaunganisha wavuvi wadogo na wadau wengine wa sekta ya uvuvi, pamoja na kuhakikisha sauti zao zinasikika katika masuala ya usimamizi wa rasilimali za baharini.

Kwa Ngatunga, utafiti wa samaki na usimamizi endelevu wa rasilimali za baharini ni maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele, hasa kwa kuwa bado kuna viumbe wengi ambao hawajatambuliwa kikamilifu na hivyo kuhitaji utafiti zaidi.

Hata hivyo, tafiti za hivi karibuni kuhusu rasilimali za maji na uvuvi zinaonesha kuwa Tanzania ina takriban spishi 540 za samaki. Idadi hiyo hufikia takriban spishi 850 zinapojumuishwa viumbe wengine wa majini, wakiwemo kaa na majongoo bahari.

Related articles

Recent articles