SANTIAGO, Chile
MAMIA ya madereva wa mabasi na malori nchini Chile wameingia barabarani kwa maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta.
Madereva hao wameishinikiza serikali yao kuangalia namna ya kupunguza bei ya dizeli, licha ya hali hiyo kusababishwa na vita vinavyoendelea kati ya Marekani na Iran.
Katika hoja yao ya msingi, waandamanaji hawakubaliani na kupanda kwa asilimia 74 kwa bei ya mafuta ya dizeli.
Baada ya maandamano hayo, Serikali ya Chile iliwaita mezani madereva hao na kuzungumza nao lakini hatua hiyo haikuzaa mwafaka.
Kwa mujibu wa taarifa, maandamano hayo yameratibiwa na Chama cha Madereva wa Malori nchini humo, Fuerza del Norte trade union.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Uchumi, Daniel Mas, ameitisha mazungumzo mengine, ingawa amesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa endapo hali itaendelea kuwa mbaya.
Wakati huo huo, Rais wa nchi hiyo ya Amerika ya Kusini, Jose Antonio Kast, amekuwa kwenye wakati mgumu tangu bei ya mafuta ilipopanda duniani kote.


