Na Editha William, Gazetini – KAGERA
MASHINDANO ya soka ya Muhaj Cup 2026 yameanza rasmi leo Novemba 11 kwa matokeo ya sare ya kutokufungana kati ya Omukishenye FC na Furniture FC.
Akizungumza baada ya dakika 90 za kugawana pointi, Kocha wa Omukishenye FC, Jacob Charles, amesema wamejifunza kutokana na mapungufu yaliyojitokeza na kuahidi kuyafanyia kazi ili kupata matokeo mazuri katika mchezo ujao.
Charles amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaahidi kuwa katika mchezo unaofuata kikosi chake kitapambana kuhakikisha kinapata ushindi na kuondoka na alama zote tatu.
Kwa upande wake, Katibu wa Mashindano ya Muhaj Cup 2026, Sharifu Idirisa, amesema mashindano hayo yanahusisha jumla ya timu nne kutoka katika mitaa minne ya Kata ya Hamgembe.


