14.2 C
New York

JET: Zipeni kipaumbele habari za uchumi wa buluu, maisha ya watu

Published:

Na Faraja Mulungu, Gazetini

WAANDISHI wa habari nchini hususan wa mazingira, wametakiwa kuboresha uandishi wa habari hizo kwa kuangazia zaidi uchumi wa buluu na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, ili kuonesha namna masuala hayo yanavyogusa maisha ya wananchi na maendeleo ya uchumi.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo, wakati akiwasilisha mada kwenye warsha iliyoandaliwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), iliyowakutanisha wadau wa mazingira, wakiwamo waandishi wa habari, mkoani Morogoro.

Chikomo amesema waandishi wanapaswa kwenda zaidi ya maelezo ya kawaida katika kuandika habari za mazingira, kwa kuangalia namna masuala hayo yanavyogusa maisha ya watu, uchumi na maendeleo ya jamii.

“Waandishi wa habari wanapaswa kwenda zaidi ya maneno ya kawaida katika kuandika habari za mazingira, kwa kuangalia namna masuala hayo yanavyogusa maisha ya watu na uchumi,” amesema Chikomo.

Kwa mujibu wa Chikomo, habari kuhusu rasilimali za bahari, ikiwemo uvuvi, kilimo cha mwani, nyasi bahari na uchafuzi wa bahari, zinapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi katika vyombo vya habari.

Ameeleza kuwa uandishi wa habari hizo unapaswa kuonesha athari za mabadiliko ya mazingira kwa kipato cha wavuvi, upatikanaji wa chakula, ajira na maisha ya jamii zinazoishi maeneo ya pwani.

Aidha, amewataka waandishi kutumia takwimu, tafiti na zana za kidijitali katika kukusanya na kuthibitisha taarifa, badala ya kutegemea madai yasiyochunguzwa.

Katika hatua nyingine, Chikomo amesisitiza umuhimu wa wanahabari kuchunguza madai ya kampuni kuhusu utunzaji wa mazingira, akieleza kuwa baadhi ya taasisi zinaweza kujionesha kuwa zinazingatia mazingira huku zikificha athari hasi za shughuli zao, hali inayojulikana kama bluewashing.

“Ni muhimu kwa waandishi kuchunguza madai ya kampuni kuhusu utunzaji wa mazingira na kutumia takwimu pamoja na ushahidi, ili kubaini ukweli na kuepuka bluewashing,” amesema Chikomo.

Ameongeza kuwa waandishi wanapaswa kueleza dhana za kitaalamu kama uchumi wa buluu, uendelevu na masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG) kwa lugha rahisi inayoweza kueleweka na wananchi.

Chikomo amesisitiza kuwa habari bora za mazingira zinahitaji kuunganisha takwimu na ushahidi pamoja na simulizi za watu wanaoathirika moja kwa moja, ili kuifanya jamii ielewe umuhimu wa kulinda na kutumia rasilimali hizo kwa uendelevu.

Akizungumzia manufaa ya mafunzo hayo, mmoja wa washiriki, Stella Aaron, mwandishi wa habari wa gazeti la Jamhuri, amesema mafunzo hayo yameonesha umuhimu wa vyombo vya habari kutumia nafasi yake kuelimisha jamii kuhusu masuala ya mazingira na athari zake katika maisha ya wananchi.

“Kupitia uandishi wenye ushahidi na taarifa sahihi, wanahabari wanaweza kuongeza uelewa wa umma, kuimarisha uwajibikaji na kuchochea usimamizi bora wa rasilimali za mazingira kwa manufaa ya jamii na vizazi vijavyo,” amesema Stella.

Naye Juma Mohamed, kutoka Clouds Media, amesema mafunzo hayo yamekuwa muhimu kwa kuwa yamemuongezea maarifa, hususan namna ya kuhusisha masuala ya mazingira na maisha ya watu katika uandishi wa habari.

“Mafunzo haya yametufungua zaidi katika kuelewa umuhimu wa kuandika habari za mazingira kwa kuhusisha athari zake kwa maisha ya wananchi, uchumi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari. Pia yametukumbusha umuhimu wa kutumia takwimu na ushahidi katika kuhakikisha tunatoa habari sahihi zenye manufaa kwa jamii,” amesema.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano WWF, Joan Itanisa. 

Shirika la WWF limekuwa mdau muhimu katika juhudi za uhifadhi wa mazingira na wanyamapori nchini Tanzania, pamoja na kuchochea matumizi endelevu ya rasilimali za asili na kupunguza athari za shughuli za kibinadamu katika mifumo ya ikolojia tangu lilipoanza shughuli zake nchini mwaka 1962.

Related articles

Recent articles