ABUJA, Nigeria
KITUO cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa nchini Nigeria (NCDC) kimeidhinisha malipo ya dharura ya Naira 100,000 takribani Sh 200,000skwa kila mtu kwa wiki kwa watu wanaowekwa karantini au kutengwa na wengine, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti mlipuko wa Ebola katika Eneo la Utawala la Shirikisho (FCT).
Mkurugenzi Mkuu wa NCDC, Dk. Jide Idris, ameeleza hayo leo Jumapili, Oktoba 25, 2026 wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Abuja, akisema hatua hiyo inalenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa watu wanaofuatiliwa na mamlaka za afya na kuwahamasisha kushirikiana na wataalamu katika kudhibiti maambukizi.
Kwa mujibu wa Idris, uamuzi huo umefikiwa baada ya baadhi ya watu waliokutana na wagonjwa au wanaofuatiliwa kuwasilisha malalamiko kuhusu gharama za chakula, malazi na namna ya kuhudumia familia zao wanapokuwa chini ya uangalizi wa afya.
“Tulianzisha malipo hayo baada ya baadhi ya watu waliokutana na wagonjwa kueleza wasiwasi kuhusu chakula, malazi na jinsi ya kuzihudumia familia zao wanapokuwa chini ya ufuatiliaji. Msaada huu unalenga kupunguza mzigo wao wa kifedha na kuwahamasisha kushirikiana na maafisa wa afya,” amesema Idris.
Amefafanua kuwa malipo hayo hayakuwa sehemu ya mpango wa awali wa kukabiliana na mlipuko huo, lakini yameonekana kuwa muhimu kutokana na hali ya dharura na changamoto zilizowasilishwa na watu walioathiriwa.
“Hili halikuwa limepangwa tangu mwanzo, lakini ni dharura. Tutaendelea kupitia upya mpango huu kadiri hali itakavyoendelea,” amesema.
NCDC yazitaka serikali za majimbo kujiandaa
Mbali na kutangaza msaada huo, Idris amezitaka serikali za majimbo nchini Nigeria kujiandaa mapema kwa dharura za afya ya umma kwa kuhakikisha zina rasilimali za kifedha na vifaa vinavyohitajika kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
Amesisitiza kuwa jukumu la kudhibiti milipuko ya magonjwa halipaswi kubebwa na Eneo la Utawala la Shirikisho pekee, bali linahitaji ushirikiano wa serikali za majimbo na mamlaka nyingine zinazohusika.
Hatua ya kutoa msaada wa kifedha kwa watu wanaowekwa karantini inalenga kuwezesha utekelezaji wa hatua za afya ya umma bila kuwaongezea mzigo wa gharama za maisha, ambao unaweza kuathiri ushirikiano wao na mamlaka za afya.
Hata hivyo, taarifa hiyo haijabainisha muda ambao malipo hayo yataendelea kutolewa wala idadi ya watu watakaonufaika na mpango huo.


