Na mwandishi wetu, Gazetini
WAZIRI wa Nishati, Dk. Juma Homera, ameitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuharakisha mazungumzo na kampuni ya Hongwang Tanzania Holdings (HWTZ) ya China ili kukamilisha makubaliano ya ununuzi wa megawati 200 za umeme, hatua inayolenga kuwezesha utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 mkoani Ruvuma.
Mradi huo unaokadiriwa kugharimu Sh trilioni 7.8 unatarajiwa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe na nishati ya jua, ukiwa sehemu ya uwekezaji mkubwa katika kongani ya viwanda inayohusisha pia ujenzi wa viwanda vya alumini na chuma.
Akizungumza Oktoba 23, 2026, wakati wa ziara yake katika kongani hiyo ya viwanda, Dk. Homera amesema kukamilika kwa makubaliano kati ya TANESCO na mwekezaji kutasaidia kuharakisha maandalizi ya mradi huo, ambao unatarajiwa kuchochea shughuli za uzalishaji na kuimarisha fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Ruvuma na maeneo jirani.
Amesema ameelezwa kuwa mradi huo utakuwa wa kwanza wa aina yake barani Afrika, hivyo amesisitiza umuhimu wa Tanesco kukamilisha mazungumzo ili mwekezaji aanze hatua zinazofuata za utekelezaji.
“Tumeelezwa mradi huu utakuwa wa kwanza barani Afrika. Natoa rai kwa Tanesco kuharakisha mazungumzo na mwekezaji ili kuwapatia megawati 200, ili kuanza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme unaotarajiwa kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 kwa kutumia makaa ya mawe na nguvu ya jua, ili kuchochea shughuli za uzalishaji na fursa za kijamii,” amesema Dk. Homera.
Uwezo unaotarajiwa wa mradi huo wa zaidi ya megawati 2,000 unakaribiana na ule wa Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), ambacho kina uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira yanayovutia uwekezaji, akisema mradi huo unatarajiwa kuongeza ajira kwa vijana na kupanua shughuli za uzalishaji katika mkoa huo.
Amesema kongani hiyo ya viwanda, ikijumuisha mradi wa kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 za umeme, inatarajiwa kuifanya Ruvuma kuwa miongoni mwa mikoa yenye miradi mikubwa ya kimkakati inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Kongani hii ya viwanda, ambayo pia itakuwa na mradi wa kuzalisha umeme zaidi ya megawati 2,000, itaifanya Ruvuma kuwa miongoni mwa mikoa yenye miradi mikubwa ya kimkakati inayoongeza fursa nyingi za kijamii na kiuchumi pamoja na ajira zaidi ya 5,000 kwa vijana,” amesema Brigedia Jenerali Abbas.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco anayeshughulikia Mipango, Utafiti na Uwekezaji, Mhandisi Amos Kaihula, amesema shirika hilo liko katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kusaini makubaliano ya ununuzi wa megawati 200 kutoka kwa mwekezaji huyo.
Amesema makubaliano hayo yatakapokamilika, yatamwezesha mwekezaji kuendelea na mchakato wa ujenzi wa mradi huo, huku Tanesco ikitarajiwa kununua sehemu ya umeme utakaokuwa ukizalishwa.
Mradi huo unatarajiwa kujengwa na kampuni ya HWTZ, chini ya kampuni mama ya HWHG ya China, na ni sehemu ya uwekezaji wa kongani ya viwanda mkoani Ruvuma unaolenga kuimarisha uzalishaji wa umeme na shughuli za viwanda.


