Na Faraja Mulugu, Gazetini
ASASI ya mazingira na afya ya AGENDA for Environment and Responsible Development (AGENDA) imetoa wito kwa Serikali kuimarisha udhibiti wa rangi zenye madini ya risasi nchini, ikionya kuwa kuendelea kwa uzalishaji, uingizaji na usambazaji wa bidhaa hizo bila udhibiti madhubuti kunaweza kuhatarisha afya za wananchi na mazingira.
AGENDA imesema licha ya hatua zilizopigwa katika kupunguza uwepo wa madini hayo kwenye rangi, bado kuna bidhaa zenye viwango vikubwa vya risasi zinazohitaji hatua za haraka kutoka kwa mamlaka za udhibiti, wazalishaji na wafanyabiashara.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam Oktoba 21, 2026, na Katibu Mtendaji wa AGENDA, Dorah Swai, wakati wa Wiki ya Kimataifa ya Kuzuia Madhara ya Sumu ya Risasi, ambapo asasi hiyo imesisitiza umuhimu wa kuhamisha nguvu kutoka kubaini uwepo wa risasi kwenye rangi kwenda kwenye hatua za kuzuia uzalishaji na matumizi ya bidhaa zisizokidhi viwango vya usalama.

Dorah amesema, kutambua rangi zenye madini ya risasi pekee hakutoshi; ni wakati wa kuongeza kasi ya kuzuia uzalishaji, uingizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya rangi hizo kwa kuimarisha udhibiti na utekelezaji wa sheria na viwango vinavyohusika.
“Matokeo ya upimaji wa sampuli za rangi uliofanyika Juni 2026 yanaonesha kuwa zaidi ya asilimia 85 ya rangi zilizopimwa hazikuwa na madini ya risasi, huku takribani asilimia 13 zikiwa na viwango vikubwa vya madini hayo,” amesema Dorah.
Amesema takwimu hizo zinaonesha mabadiliko ikilinganishwa na mwaka 2009, ambapo ni asilimia 23 pekee ya rangi zilizopimwa zilizokuwa hazina risasi. Hata hivyo, uwepo wa bidhaa zenye viwango vikubwa vya madini hayo unaashiria kuwa bado kuna changamoto katika kuhakikisha rangi zote zinazouzwa nchini zinakidhi matakwa ya usalama.
Asasi hiyo imezisihi mamlaka husika kuongeza ukaguzi katika viwanda, mipakani na maeneo ya biashara, pamoja na kuchukua hatua dhidi ya bidhaa zinazokiuka kiwango cha ukomo wa risasi cha sehemu 90 kwa kila milioni (90 ppm).
Aidha, imesisitiza kuwa wazalishaji na waagizaji wana wajibu wa kuhakikisha bidhaa zao hazina viwango hatarishi vya risasi, ikieleza kuwa viambato mbadala visivyo na madini hayo vinapatikana na vinaweza kutumika kutengeneza rangi salama.
Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Hamadi Taimuru, amesema Serikali inaendelea kufuatilia matumizi ya madini ya risasi kutokana na uwezo wake wa kujikusanya mwilini na kusababisha madhara kwa afya ya binadamu.

Amesema risasi ni miongoni mwa madini mazito (heavy metals) ambayo hayana kazi ya manufaa mwilini, lakini yanapoingia katika mwili wa binadamu yanaweza kuathiri mifumo mbalimbali ya afya, hasa pale mtu anapokutana nayo mara kwa mara.
“Serikali haiwezi kufumbia macho kemikali ya namna hii. Ndiyo maana tunaifuatilia kwa karibu katika kila eneo ambako inazalishwa au kutumika, ili kuhakikisha matumizi yake hayasababishi madhara kwa jamii yetu,” amesema Taimuru.
Ameeleza kuwa watoto wadogo wako katika hatari kubwa zaidi ya kuathiriwa na risasi kutokana na athari zake kwa ukuaji wa ubongo, uwezo wa kufikiri na kujifunza. Kwa watu wazima, kuathiriwa na risasi kunaweza kuharibu figo na kuathiri mfumo wa uzazi, ikiwamo kupunguza idadi ya mbegu za kiume. Kwa wanawake wajawazito, kunaweza kuongeza hatari ya mimba kuharibika na kujifungua kabla ya wakati.
Aidha, amewataka wananchi wanaojihusisha na shughuli zinazotumia madini hayo kuchukua tahadhari, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa shughuli hizo ili kulinda afya za wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kubdhibiti Matukio na sumu Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Yohana Geoshashy, amesema upatikanaji wa takwimu za watu walioathiriwa na sumu ya risasi nchini ni changamoto, kwa sababu dalili za kuathiriwa na madini hayo zinaweza kufanana na zile za magonjwa mengine.
Ameeleza kuwa matatizo ya figo, upungufu wa damu na changamoto za ukuaji wa watoto yanaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, hivyo ni muhimu kuzingatia historia ya mtu ya kukutana na risasi pamoja na kufanya vipimo vinavyoweza kuthibitisha uwepo wake mwilini.
“Uwezo wa kupima risasi mwilini na kubaini kiwango cha madhara yake haupatikani kwa urahisi katika vituo vyote vya afya nchini, hali inayochangia ugumu wa kupata takwimu sahihi za watu walioathiriwa.
“Watu wanaofanya kazi katika mazingira yenye risasi, wakiwamo wanaorejesha madini hayo na mafundi wanaopaka rangi, wanapaswa kuchukua tahadhari na kujiepusha na kuendelea kukaa katika mazingira hatarishi wanapobainika kuathiriwa,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha udhibiti wa bidhaa zinazoingia sokoni, zikiwamo rangi, vipodozi na vifaa vya kuchezea watoto, ili kupunguza uwezekano wa wananchi kukutana na kemikali hatarishi kupitia bidhaa wanazotumia kila siku.
Naye David Elisha, Mkufunzi kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), amesema matumizi ya vifaa vya kujikinga ni muhimu, lakini yanapaswa kuwa hatua ya mwisho baada ya kuchukua hatua nyingine za kuondoa au kupunguza vihatarishi katika mazingira ya kazi.
Amesema sheria ya usalama na afya mahali pa kazi inawataka wazalishaji na wasambazaji kutoa taarifa kuhusu viambato vya bidhaa wanazozalisha au kusambaza, madhara yake na namna salama ya kuzitumia, kupitia nyaraka za taarifa za usalama wa kemikali (Safety Data Sheets).
“Udhibiti wa risasi unapaswa kuanza kwa kuondoa kiambato hicho hatari kwenye bidhaa pale inapowezekana, badala ya kutegemea vifaa kinga pekee, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaendana na msimamo wa AGENDA wa kuhamia kutoka utambuzi wa tatizo kwenda kwenye kinga,” amesema Elisha.
Ameongeza kuwa OSHA imekuwa ikifanya ukaguzi na uchunguzi wa afya za wafanyakazi katika baadhi ya sekta rasmi, ikiwamo viwanda vya rangi, ili kubaini mapema madhara yanayoweza kujitokeza na kuwashauri waajiri kuchukua hatua za kuwalinda wafanyakazi.
Hata hivyo, amesema wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi, wakiwamo mafundi wa mitaani wanaopaka rangi nyumba na magari, wanahitaji kupewa elimu zaidi kwa sababu wengi hufanya kazi kwa mazoea bila kutumia vifaa kinga au kutambua madhara ya muda mrefu ya kemikali wanazokutana nazo.
Amesisitiza kuwa elimu kwa wananchi, ushirikiano wa taasisi za Serikali na wadau wa mazingira ni muhimu katika kufikia makundi hayo na kulinda afya ya nguvu kazi ya taifa.
AGENDA imesema imekuwa ikifanya kazi kwa miaka 17 kwa kushirikiana na Serikali, viwanda vya rangi na wadau wa kimataifa katika kufanya tafiti, kupima sampuli za rangi na kuelimisha umma kuhusu madhara ya risasi.
Wadau hao ni pamoja na International Pollutants Elimination Network (IPEN) na Lead Exposure Elimination Project (LEEP), wanaoshiriki katika juhudi za kupunguza na kuondoa matumizi ya risasi katika rangi.
Asasi hiyo imetaka mamlaka husika kutekeleza Mpango wa Kuondoa Rangi Zenye Madini ya Risasi Tanzania ulioandaliwa Juni 2026 kwa ushiriki wa mamlaka zinazohusika, ili kuimarisha usimamizi wa viwango vya usalama na kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka matakwa yaliyowekwa.
Katika msimamo wake, AGENDA imesema: “AGENDA inaamini kuwa ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi, wataalamu, vyombo vya habari na wananchi ni msingi muhimu wa kufanikisha Tanzania isiyo na rangi zenye madini ya risasi.”
Wito huo umetolewa wakati wa Wiki ya Kimataifa ya Kuzuia Madhara ya Sumu ya Risasi, inayoadhimishwa kila mwaka mwezi Oktoba tangu mwaka 2013. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kutoka Kutambua Kwenda Kuzuia,” inayosisitiza umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti baada ya kubaini chanzo cha hatari.
AGENDA imetoa wito kwa Serikali, wazalishaji, wafanyabiashara na wananchi kushirikiana kuhakikisha rangi zenye viwango hatarishi vya risasi zinaondolewa sokoni, kwa lengo la kulinda afya za watoto, jamii kwa ujumla na mazingira.


