22.2 C
New York

Vigogo walioiingiza matatani Man City

Published:

MANCHESTER, Uingereza

KLABU ya Manchester City iko kwenye presha kubwa kutokana na mashitaka inayokabiliwa nayo. Mashitaka ya kukiuka nidhamu ya matumizi ya fedha. Huenda ikakatwa pointi, kupokonywa mataji, na hata kushushwa daraja.

Nyuma ya changamoto hiyo, wapo viongozi kadhaa wenye ushawishi mkubwa klabuni hapo. Kwamba kama kuna shida yoyote, basi walihusika kwa kiasi kikubwa.

Dkt. Sulaiman Al-Fahim

Alikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya Kampuni ya Abu Dhabi United Group iliyoinunua Man City mwaka 2008. Ndiye aliyesimamia mazungumzo ya ununuzi wa klabu hiyo kwa Pauni milioni 200.

Baadaye, Dkt. Al-Fahim alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani kwa kosa la kumuibia mkewe kitita cha Pauni milioni 5 alichokitumia kuinunua klabu ya Portsmouth.

Khaldoon al-Mubarak

Aliwahi kushika nafasi mbalimbali za kiuongozi katika Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu [UAE]. Amekuwa Mwenyekiti wa klabu ya Man City tangu walipoinunua mwaka 2008.

Al-Mubarak mwenye umri wa miaka 51, pia ndiye Mwenyekiti wa City Football Group (CFG), kampuni ambayo ndiyo inayoimiliki klabu ya Man City.

Sheikh Mansour bin Zayed Al Nahyan

Ni Makamu wa Rais na Naibu Waziri Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu [UAE]. Ni sehemu ya familia ya Kifalme ya nchi hiyo. Amekuwa ndiye mmiliki wa Man City tangu mwaka 2008.

Taarifa zimekuwa zikidai kuwa tajiri huyo amekuwa akiwapa fedha wafanyabiashara wa UAE ili wawekeze katika klabu yake hiyo ya Ligi Kuu ya England.

Garry Cook

Baada ya matajiri kuinunua Man Citry mwaka 2008, Cook aliajiriwa na kupewa nafasi ya Mtendaji Mkuu wa klabu. Alijiuzulu wadhifa huo mwaka 2012.

Sababu ya kujizulu ni taarifa zilizodai kuwa alimtumia ujumbe wa baruapepe [enail] mama mzazi wa beki Nedum Onuoha akimdhihaki baada ya kupata ugonjwa wa saratani.

Simon Pearce

Amekuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Man City tangu klabu hiyo iliponunuliwa mwaka 2008. Kwa upande mwingine, ana nafasi nyeti kwa mabosi wa klabu hiyo.

Ndiyo, Pearce ni mshauri mkuu wa Executive Affairs Authority, Shirika la Serikali ya Abu Dhabi linalomshauri Rais wa UAE, Mohamed bin Zayed Al Nahyan. Pia, ndiye Makamu wa Rais wa Melbourne City, klabu nyingine inayomilikiwa na CFG.

Related articles

Recent articles