MOSCOW, Urusi
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin, ameimarisha vita vyake na Ukraine baada ya kutangaza ajira za wananjeshi wapya 15,500. Ni miaka minne na nususasa tangu nchi jirani hizo zilipoingia kwenye vita Februari, 2022.
Aidha, hii ni mara ya nne ndani ya mwaka huu kwa Rais Putin kuongeza ukubwa wa jeshi lake na wameajiriwa wanajeshi 47,860 kwa kipindi cha miezi sita ya hivi karibuni.
Pande zote mbili, kwa maana ya Urusi na Ukraine, zimekuwa zikitegemea mashambulizi ya mbali, pamoja na matumizi makubwa ya teknolojia ya ndege zisizo na rubani [drones].
Hata hivyo, si Rais Putin wala mamlaka za Urusi zilizoeleza sababu iliyosukuma kiongozi huyo kuendelea kuongeza ukubwa wa jeshi, ingawa hatua hiyo inaashiria kwamba bado vita vina muda mrefu kumalizika.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Mambo ya Nje la Urusi, Andrei Kortunov, anaona hatua ya Rais Putin inafifisha matumaini ya nchi hizo kumaliza vita kwa njia ya kidiplomasia. “Hali ni mbaya kwa upande wa suluhu ya kidiplomasia,” amesema.
Kwa upande mwingine, uamuzi wa kuongeza jeshi umetafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kuwa ni hali mbaya wanayopitia Urusi mbele ya maadui zao, Ukraine.
Akifafanua hilo, mtaalamu wa masuala ya usalama nchini Ukraine, Olena Halushka, anaamini Urusi ‘imevurugwa’ kwa kuona haijafanikisha malengo yao ya vita.
“Mwaka jana, katika Mkutano wa Anchorage [uliofanyika katika Jimbo la Alaska nchini Marekani], Putin aliendelea kuishinikiza Ukraine kuondosha majeshi yake katika Mji wa Donetsk [Ukraine].
“Alidai kuwa Ukraine ingekiona cha moto punde endapo ingeendelea kung’ang’ania. Ni mwaka umepita na bado hali imebaki ile ile [Ukraine haijaacha kudhibiti Donetsk],” amesema Halushka, ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Kituo cha Kudhibiti Rushwa mjini Kyiv.
Hivi karibuni, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, alisema Urusi kwa sasa imechanganyikiwa na kuanza kuajiri wapiganaji wa nje, akitaja idadi ya wanajeshi 8,000 kutoka Korea ya Kaskazini.
Katika taarifa ya Ukraine inayoungwa mkono na Korea ya Kusini, Urusi imeshapokea wanajeshi kati ya 14,000 na 15,000 kutoka Korea ya Kaskazini ili kuisaidia katika uwanja wa vita. Madai hayo yamekanushwa mara zote na mamlaka za Urusi.
Vita vya Urusi na Ukraine vimeendelea kushuhudia mashambulizi ya mara kwa mara katika nchi hizo. Jumatatu ya wiki hii, watu takribani 10 walipoteza maisha na wengine 80 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya Urusi.
Ndege zisizo na rubani za Urusi zilishambulia Chuo cha Sayansi mjini Kyiv, pamoja na kushambulia miji ya Dnipro, Kharkiv, Zaporizhia na maeneo mbalimbali nchini Ukraine.
Wakati huo huo, operesheni za kijeshi za Ukraine zimeendelea kudhibiti maeneo ya Kaskazini mwa Mji wa Donetsk. Mmoja ya viongozi waandamizi wa jeshi amesema tayari wanashikilia eneo lenye ukubwa wa kiliometa za mraba 176.
Licha ya vita kuendelea, zimekuwapo jitihada za kidiplomasia zikiongozwa na Serikali ya Marekani. Mwanzoni mwa mwezi huu [Septemba, 2026], wawakilishi wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, walifunga safari hadi Moscow na kisha Kyiv.
Katika ziara yao hiyo, walikutana na kufanya mazungumzo na Putin na Zelenskyy kwa nyakati tofauti, ingawa mvutano juu ya umiliki wa ardhi ulionekana kuwa kizingiti cha pande mbili hizo kufikia mwafaka.
Ukraine inataka Urusi iondoshe majeshi yake nchini humo. Urusi, kwa upande wake, inaamini Ukraine ni mali yao, hivyo ina mamlaka ya kudhibiti baadhi ya maeneo.
Lakini, zipo taarifa zilizothibitishwa na Zelenskyy zikidai kuwa Marekani imeandaa mkutano utakaozikutanisha meza moja Urusi na Ukraine na unatarajiwa kufanyika Umoja wa Falme za Kiarabu [UAE].
Mwisho, kauli ya Putin aliyesema kuna manufaa makubwa kwa Urusi kuendelea na vita kuliko kufikia mwafaka imeibua hisia kwamba bado kuna safari ndefu katika kusaka suluhu.


