19.2 C
New York

Lake Energies yazindua mfumo wa kujihudumia mafuta kidijitali

Published:

Na Faraja Mulungu, Gazetini

KAMPUNI  ya Lake Energies imezindua mfumo wa kidijitali unaowawezesha wateja kujihudumia wenyewe katika vituo vya mafuta, hatua inayolenga kupunguza muda wa kupata huduma na kuongeza matumizi ya teknolojia katika sekta ya mafuta nchini.

Mfumo huo umeanza kutumika katika kituo cha Selander, jijini Dar es Salaam, kuanzia Oktoba 1, 2026.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Uendeshaji wa Lake Energies, Juma Nour, amesema wazo la kuanzisha mfumo huo limetokana na maono ya Mwenyekiti wa Lake Group, Ali Edha Awadh, ya kuona Tanzania na Afrika Mashariki zikisonga zaidi katika matumizi ya teknolojia na huduma za kidijitali.

Amesema mfumo huo unamwezesha mteja kufika kituoni, kufanya malipo na kujihudumia bila kusubiri mhudumu wa pampu kumhudumia moja kwa moja.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, mfumo huo unalenga kupunguza muda ambao mteja hutumia kupata huduma, huku wahudumu wa pampu wakiendelea kuwepo kwa ajili ya kuwasaidia wateja wanaohitaji maelekezo au msaada wa kutumia mfumo huo.

“Mtu anaweza kufika kituoni akajihudumia mwenyewe. Mfumo huu utasaidia kupunguza muda wa kupata huduma, lakini pia wahudumu wataendelea kuwepo katika vituo kwa ajili ya kuwasaidia wateja pale inapohitajika,” amesema Nour.

Amesema mfumo huo pia unalenga kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma, kwa kuwa mteja hahitaji kusubiri mhudumu ili kuanza mchakato wa malipo na kupata mafuta.

“Utakapofika kwenye mashine utaweza kujihudumia mwenyewe, kufanya malipo, kupata mafuta na kuendelea na safari yako bila kikwazo cha kusubiri mhudumu,” amesema.

Malipo kwa simu na QR Code

Mkuu wa Ubunifu wa kampuni hiyo, Salim Alifahd, amesema mfumo huo umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya watumiaji wenye aina tofauti za simu.

Mwenyekiti wa Lake Group, Ali Edha Awadh(kushoto) akipata maelezo namna mfumo huo unavyofanya kazi kutoka kwa Mkuu wa Ubunifu Lake Group, Salim Alifahd, wakati wa hafla ya uzinduwi iliyofanyika Oktoba 1, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema wateja wenye simu janja wanaweza kutumia QR Code kufanya malipo, huku wale wasio na simu janja wakiweza kutumia simu zao za kawaida kufanya malipo na kupata huduma.

“Watumiaji wa huduma za benki zinazowezesha malipo kwa QR Code wanaweza kutumia programu zao za benki kufanya malipo na kisha kuendelea na huduma ya kujihudumia,” amesema Alifahd.

Ajira za wahudumu kuendelea

Naye Msaidizi wa Mauzo kwa Wateja Wadogo wa Lake Energies, Renatus Hemed, amesema kuanzishwa kwa mfumo huo hakumaanishi kuondolewa kwa ajira za wahudumu wa pampu.

Amesema wahudumu wataendelea kuwepo katika vituo kwa ajili ya kuwasaidia wateja, hususan wale wanaohitaji maelekezo kuhusu matumizi ya mfumo huo.

Amesema mfumo huo ni sehemu ya jitihada za kampuni hiyo kuunga mkono matumizi ya teknolojia na huduma za kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Tunataka Watanzania wapate hisia kwamba nasi tupo katika hatua ambayo dunia imefikia katika matumizi ya teknolojia. Tunataka kuendelea kuivuta Tanzania ifikie kiwango hicho,” amesema.

Mfumo kupanuliwa

Kwa mujibu wa kampuni hiyo yenye vituo vya mafuta zaidi ya 150 nchi nzima, kituo cha Selander ni cha kwanza kutumia mfumo huo nchini Tanzania, huku ikipanga kuupeleka katika vituo vingine vya Dar es Salaam na baadaye mikoa mingine nchini.

Hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma na kurahisisha upatikanaji wa huduma za mafuta kwa wateja.

Related articles

Recent articles