25.2 C
New York

TCDC vawaonya viongozi wa Ushirika dhidi ya ubadhilifu

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini-Njombe

TUME ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) imewataka viongozi na watumishi wa vyama vya ushirika nchini kuepuka vitendo vya ubadhilifu na kuzingatia sheria na taratibu za ushirika ili kuimarisha vyama hivyo na kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wito huo umetolewa na Ofisa Ushirika wa TCDC anayeshughulikia vyama vya kifedha, Stiven Kalabo, wakati wa kliniki ya TCDC inayofanyika mjini Njombe kwa lengo la kutoa elimu, kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wanachama wa vyama vya ushirika na wananchi.

Kalabo amesema Tume imeamua kuwafikia wanachama moja kwa moja ili kuwasikiliza, kutoa elimu kuhusu masuala ya ushirika pamoja na kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Amesema viongozi na watumishi wa vyama vya ushirika wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuzingatia sheria na taratibu za ushirika ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Viongozi na watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria na taratibu za ushirika ili kuepuka kukutana na mkono wa sheria,” amesema Kalabo.

Kwa upande wake, mwanachama wa vyama vya ushirika, Anna Kitindi, amesema vitendo vya ubadhilifu pamoja na changamoto nyingine vimekuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha vyama vya ushirika mkoani Njombe.

Kitindi ameiomba Serikali kuendelea kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaobainika kujihusisha na vitendo vya ubadhilifu, akisema hatua hiyo itasaidia kurejesha imani ya wanachama na kuimarisha vyama vya ushirika.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Juma Sweda, amesema vyama vya ushirika vimekuwa vikikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimesababisha baadhi yao kushindwa kuendelea na shughuli zao na hatimaye kufa.

“Vyama vyetu vya ushirika vina changamoto nyingi na vyama vingi vilivyopitia changamoto vilikufa, lakini kwa sasa Tume ya Ushirika imejipanga kuhakikisha inafufua vyama vya ushirika,” amesema Sweda.

Related articles

Recent articles