LONDON, Uingereza
KWA sasa, kinda wa Arsenal, Max Downman, ni mchezaji wa pili [baada ya Wayne Rooney] kuifungia klabu ya England mabao mawili ya mchezo mmoja akiwa na mwenye umri wa miaka 16.
Dowman aliyeanza kuitumikia Arsenal mwaka jana, aliweka rekodi hiyo baada ya mabao yake mawili katika mchezo wa Carabao Cup dhidi ya Ipswich Town. Rooney alifanya hivyo akiwa na Man United mwaka 2002 katika mechi dhidi ya Everton.
Pili, Dowman ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Aliikabili Slavia Prague [2025] akiwa na miaka 15 na siku 308.
Tatu, ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao Ligi Kuu ya England [EPL]. Aliweka rekodi hiyo Machi, 2026, alipoifunga Everton akiwa na miaka 16 na siku 73.
Nne, ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kutwaa ubingwa wa EPL. Msimu uliopita, 2025-26, Arseal walibeba ‘ndoo’ hiyo akiwa na miaka 16 na siku 144.
Tano, ndiye mchezaji mdogo zaidi kuanza kikosini katika historia ya EPL. Ni katika mchezo wa mwisho wa msimu wa 2025-26, ambapo aliivaa Crystal Palace akiwa na miaka 16 na siku 144.
Sita, ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuifungia bao Arsenal. Aliifunga Everton na kuivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na mkongwe wao, Cesc Fabregas.
Saba, mchezaji mdogo zaidi kuingia ‘first eleven’ ya Arsenal. Aliweka rekodi hiyo alipoanza dhidi ya Brighton katika mchezo wa Carabao Cup akiwa na miaka 15 na siku 302.
Nane, Dowman ndiye mchezaji mdogo zaidi kutumika katika vikosi vya timu za vijana za U-18 na U-21 za klabu yake ya Arsenal.
Tisa, Dowman ndiye mchezaji mdogo zaidi kufunga bao katika U-19 ya England, akivunja rekodi ya Ryan Sessegnon. Alifunga katika ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Wales.
Mwisho, Dowman ni kipenzi cha kocha Mikel Arteta na ameahidi kumpa nafasi zaidi msimu huu. “Ni mchezaji mzuri. Anaweza kufika mbali zaidi endapo ataendeleza hiki anachokifanya,” amesema Arteta.


