Na mwandishi wetu, Gazetini
SERIKALI imesema katika kuongeza ufanisi katika sekta za Bandari nchini kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya uhudumiaji wa shehena ili kuongeza ufanisi katika sekta ya Uchukuzi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Dk. Rashid Chuachua kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo wakati akifungua kikao cha Wadau wa Sekta ya Usafirishaji – Ushoroba wa Kati kilichofanyika Septemba 16,2026 mkoani humo.
Dk.Chuachua amesema anaamini mijadala itakayoibuka itakuja na ufumbuzi wa changamoto katika usafirishaji kupitia Ushoroba wa Kati.
Katika salamu zake za ukaribisho Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Dk. Baraka Mdima amesema Ushoroba wa Kati ni moja kati ya mihimili muhimu ya biashara,si kwa Kigoma pekee bali kwa Taifa zima kwani umekuwa daraja la kuiunganisha Tanzania na nchi zingine katika uchukuzi wa shehena.
Aidha Dk. Mdima amesema jumla ya shehena iliyohudumiwa na Bandari zote zinazosimamiwa na TPA kwa mwaka wa fedha uliopita ilifikia tani milioni 39.898 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 21.8 ukilinganisha na mwaka uliotangulia.
Dk.Mdima amesema kikao cha Wadau wa Ushoroba wa Kati kimeandaliwa mahususi kabisa ili kwa pamoja tupate fursa ya kujifanyia tathimini ya tulichokifanya mwaka uliopita na kutafakari namna bora kuboresha ili kuongeza ufanisi katika sekta ya Uchukuzi nchini.
Akizungumza mapema Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula amesema Serikali kupitia TPA imefanya uwekezaji wa zaidi ya bilioni 100 ili kutengenza mazingira wezeshi ya kuhudumia shehena inayopita katika Bandari ya Kigoma.
Akiongea kuhusu kuongezeka kwa shehena, Mabula amesema imeongezeka kutoka zaidi ya tani 200,000 mpaka kufikia tani 815,285 kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 na baada ya maboresho matarajio ni kufika mpaka tani milioni 2.



