LONDON, Uingereza
UMESHAWAHI kusikia msemo maarufu katika soka usemao ‘usajili ni kamari?’ Si kila mchezaji anayesajiliwa, iwe hata kwa pesa nyingi, ataweza kung’ara katika klabu anayojiunga nayo.
Wengi hufeli kuendeleza makali waliyokuwa nayo huko walikotoka lakini kwa wachezaji hawa, stori ilikuwa tofauti. Walikuwa wakubwa zaidi katika klabu zao mpya.
PETR CECH [RENNES – CHELSEA]
Chelsea walitumia Pauni milioni 7 tu kumng’oa Rennes ya Ufaransa mwaka 2004. Cech aliruhusu mabao 15 tu na ‘clean sheet’ 24 katika msimu wake wa kwanza EPL.
Hakuishiah apo. Kipa huyo raia wa Jamhuri ya Czech, aliitumikia Chelsea kwa misimu 11, akiipa mataji manne ya EPL na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
ALAN SHEARER [SOUTHAMPTON – BLACKBURN]
Ikiwa imepanda Daraja mwaka 1992, Blackburn ilivunja rekodi ya usajili wa EPL kwa kumchukua Shearer, ambaye alikuwa kwenye mtego wa Manchester United.
Shearer alifunga mabao 16 katika mechi 21 za msimu wake wa kwanza EPL. Msimu uliofuata, alifunga mara 31 na Blackburn kumaliza katika nafasi ya pili. Msimu uliofuata, alifunga 34 na timu hiyo ikawa bingwa.
CARLOS TEVEZ [CORINTHIANS – WEST HAM]
Ni usajili wa mwaka 2006, ambapo Tevez aliongozana na Muargentina mwenzake, Javier Mascherano, kujiunga na West Ham iliyokuwa chini ya kocha Alan Pardew.
Msimu wake wa kwanza, West Ham ikiwa kwenye nafasi za kushuka daraja, Tevez aliiokoa kwa mabao yake saba katika mechi 11 za mwisho.
VIRGIL VAN DIJK [SOUTHAMPTON – LIVERPOOL]
Usajili wa Pauni milioni 75 mwaka 2018. Katika msimu wake wa kwanza, Liverpool ilipoteza mechi moja pekee, iliruhusu mabao 22 na kumaliza msimu wa EPL ikiwa na pointi 97. Walikosa ubingwa lakini walitwaa taji la Ligi ya Mabingwa.
Msimu uliofuata, Van Dijk aliendeleza moto wake kwenye eneo la ulinzi na haikushangaza kuona Liverpool ikitwaa ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 kupita.
ROBIN VAN PERSIE [ARSENAL – MAN UNITED]
Ni usajili wa mwaka 2012, ambao uliigharimu Man United kiasi cha Pauni milioni 22.5. Msimu wake wa mwisho kabla ya kwenda Old Trafford, Mholanzi huyo alikuwa mfungaji bora wa EPL.
Akiwa Man United, Van Persie alifunga mabao 26 na Man United kutwaa taji la EPL, msimu ambao ulikuwa wa mwisho kwa kocha Alex Ferguson kuinoa timu hiyo.
SOL CAMPBELL [TOTTENHAM – ARSENAL]
Arsenal walimchukua bure baada ya kumaliza mkataba wake na Spurs mwaka 2001. Campbell aliichagua Arsenal licha ya kutakiwa Barcelona, Bayern Munich na Inter Milan.
Akiwa kwenye safu ya ulinzi, Arsenal ilitwaa mataji mawili [EPL na FA] katika msimu wake wa kwanza. Msimu uliofuata, akaipa EPL bila kupoteza mechi [Invincibles].
NG’OLO KANTE [CAEN – LEICESTER]
Alitokea Caen ya Ufaransa mwaka 2015, usajili wake ukigharimu Pauni milioni 5.6. Katika msimu wa kwanza, akawa sehemu muhimu ya safu ya kiungo ya Leicester wakati timu hiyo ikitwaa taji la EPL.
Msimu huo, Kante alikosa mechi moja pekee, kisha kiwango chake cha ubingwa kikaivutia Chelsea iliyolipa mara tano ya dau lake la awali [Pauni Mi. 5.6].
SERGIO AGUERO [ATLETICO – MAN CITY]
Mwaka 2011, Atletico Madrid iliwauzia Manchester City huduma ya Muargentina huyo kwa Pauni milioni 35. Katika mechi ya kwanza tu, alifunga mara mbili na asisti moja ndani ya dakika 40 dhidi ya Swansea City.
Miezi 10 baadaye, alifunga mabao 23 katika mechi 34 na Man City kutwaa taji la EPL kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1968. Aguero aliondoka Etihad akiwa mfungaji bora wa muda wote [mabao 260], pia akibeba mataji Matano ya Ligi Kuu hiyo.
ERIC CANTONA [LEEDS – MAN UNITED]
Usajili uliogharimu Pauni milioni 1.6 tu mwaka 1992. Mfaransa huyo aliyekuwa akicheza eneo la kiungo aliondoka Leeds baada ya kukorofishana na kocha wake, Howard Wilkinson.
Katika msimu wake wa kwanza Man United, Cantona alifunga mabao tisa katika mechi 23 na Man United kuwa mabingwa wa EPL kwa tofauti ya pointi 10. Alistaafu akiwa amefunga mabao 82 katika mechi 185 alizocheza kwa miaka mitano akiwa Man United, pia akiipa mataji manne [mawili ya EPL].


