23.9 C
New York

Idi Amin; Utata wa ‘birthday’, usaliti na udikteta wake (10)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA sehemu ya tisa, tuliishia pale bi. Madina alipomuomba Yoweri Museveni amruhusu Idi Amin kurudi Uganda. Rais huyo akasema ‘Idi Amin atalipia dhambi zote alizofanya’, akimaanisha kuwa angefunguliwa mashitaka na kufungwa. Endelea …

Baada ya muda mrefu wa kuishi kwenye chumba cha wagonjwa mahututi akitumia mashine ya kupumua kutokana na tatizo la moyo, Idi Amin alifariki Agosti 16, 2003, mjini Jeddah. Alizikwa katika Makaburi ya Al Ruwais.

Miezi michache baadaye, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Uingereza (1977 – 1979), David Owen, alisema aliwahi kusuka mpango wa Idi Amin kuuawa wakati ule wa utawala wake nchini Uganda.

Katika maisha yake, Idi Amin alioa wanawake sita tofauti. Mke wake wa kwanza ni Malyamu aliyefunga naye ndoa Machi, 1962. Alioa mke wa pili, Kay, mwaka 1966. Mwaka 1967, alioa mke wa tatu, Nora, kisha akamuongeza Nalongo Madina mwaka 1972.

Machi 26, 1974, kupitia Redio ya Taifa ya Uganda, alitangaza kuwapa talaka wake zake watatu – Malyamu, Kay na Nora – na baadaye kila mmoja kwa wakati alianza kukutwa na majanga.

Malyamu alikamatwa na polisi mjini Tororo, mpakani mwa Kenya. Baadaye, Kay alifariki katika mazingira ya kutatanisha na mwili wake kuokotwa. Nora alikimbilia Zaire mwaka 1979 na hadi leo hajulikani alikoishia.

Kabla ya hapo, tayari Idi Amin alishafunga ndoa ya kifahari iliyogharimu kiasi cha Pauni milioni 2 na binti wa miaka 19, Sarah Kyolaba. Mrembo huyo alikuwa dansa wa Bendi ya muziki ya Revolutionary Suicide Mechanised Regiment.

Ndoa yao ilifungwa wakati Mkutano wa Umoja wa Afrika, AU, wakati huo ukifahamika kwa jina la OAU, uliofanyika Kampala. Mpambe wa bwana harusi (Idi Amin) alikuwa kiongozi wa Palestina wakati huo, Yasser Arafat.

Kabla ya kuolewa na Idi Amin, Sarah alikuwa akiishi na mpenzi wake, Jesse Gitta, ambaye alilazimika kuondoka Uganda na kukimbilia Kenya.

Sara, kama ilivyokuwa kwa wenzake watatu, naye hakukaa sana kwenye ndoa yake na Idi Amin. Baaadaye, alihamia Uingereza, ambako alifariki mwaka 2015 akiwa mfanyakazi wa saluni.

Hadi anafariki, Idi Amin alikuwa na watoto 40 kwa wanawake saba tofauti. Vyanzo vingine vya habari vinadai kuwa idadi kamili ni watoto 60 na mahusiano yanahusisisha wanawake zaidi ya hao saba.

Hadi mwaka 2003, mtoto wake wa kwanza wa kiume aliyezaliwa mwaka 1955, Taban Amin, alikuwa kiongozi wa West Nile Bank Front, Kundi la waasi lililokuwa likiipinga Serikali ya Yoweri Museveni.

Hata hivyo, mwaka 2005, Museveni alimchukua Taban na mwaka uliofuata alimteua kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Usalama. Mtoto wake mwingine, Haji Ali Amin, aligombea kiti cha Meya wa Halimashauri ya Njeru Mjini mwa 2002 lakini hakushinda.

Faisal Wangita, mtoto wa tatu wa ndoa ya Sarah na Idi Amin, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani mwaka 2006 kwa kujihusisha na genge maarufu la uhalifu huko Kaskazini mwa London, Uingereza.

Mwanzoni mwa mwaka 2007, iliibuka filamu iitwayo ‘The Last King of Scotland’ ambayo ilitwaa tuzo mbalimbali, ikielezea maisha ya kikatili ya utawala wa Idi Amin.

Filamu hiyo ilimchefua mtoto wake wa 10 kati ya 40, Jaffar Amin, na kuahidi angeandika kitabu cha kuisafisha taswira ya baba yake iliyochafuliwa na vyombo vya habari vya Magharibi.

NB: Hii ni sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala haya ya ‘Idi Amin; Utata wa ‘birthday’, usaliti na udikteta wake’, hivyo kama ulipitwa na sehemu zilizopita, utazipata kwa kutembelea www.gazetini.co.tz

Related articles

Recent articles