23.9 C
New York

Mykhailo Fedorov kumvaa Zelensky kiti cha urais?

Published:

KYIV, Ukraine

UKIWA ni mwezi mmoja tangu alipojiuzulu katika nafasi yake ya Waziri wa Ulinzi, Mykhailo Fedorov ameibuka na kauli zinazoashiria kuwa amejipanga kumvaa aliyekuwa bosi wake, Volodymyr Zelenskyy, katika kinyang’anyiro cha urais.

Katika video ya dakika tisa aliyoposti katika chaneli yake ya mtandao wa YouTube, Fedorov, ameeleza amesema changamoto kubwa ya Ukraine haipo kwenye wizara moja, bali uongozi mbaya wa Serikali, kauli ambayo inaibua vita kati yake na Rais Zelenskyy.

Alisema rushwa serikalini, achilia mbali kutokufanyika kwa Uchaguzi Mkuu tangu mwaka 2019, ni kielelezo cha namna mambo yalivyo mabaya katika eneo la uongozi wa juu wa nchi hiyo.

Agosti 19, 2026, Shirika la Kukabiliana na Rushwa nchini humo (NABU) liliagiza wapelelezi wake kwenda kufanya ukaguzi katika nyumba za vigogo kadhaa wa Serikali.

Katika taarifa yake, NABU ilieleza kuwa operesheni hiyo ililenga kuubaini mtandao wa uhalifu unaohusisha viongozi wa Ofisi ya Serikali.

Akizungumzia hilo, Fedorov alionya kuwa ni hatari kuona uteuzi wa nafasi za juu serikalini hauzingatii weledi, uwezo na matokeo, bali upendeleo kwa wale wanaoheshimu mamlaka.

Fedorov alifukuzwa kazi Julai 15, 2026 na siku iliyofuata maandamano makuwa ya raia katika miji mikubwa ya Kyiv, Lviv, Dnipro, Kharkiv na Zaporizhzhia yaliibuka kupinga hatua hiyo ya Rais Zelensky.

Kwa mujibu wa taasisi za utafiti, ushawishi wa Fedorov kwa raia uliongezeka kwa asilimia 30 (35% – 65%), ndani ya wiki moja tu ya maandamano hayo. Pia, utafiti ulibaini kuwa asilimia 72 ya raia wa Ukraine hawakutaka afukuzwe kazi.

Hata hivyo, mchambuzi wa siasa kutoka Taasisi ya Uchambuzi na Mikakati mjini Kyiv, Ihor Chalenko, amesema video aliyoposti Fedorov akiishutumu Serikali ni njia yake ya kujijenga kisiasa baada ya ushawishi aliovuna wakati wa maandamano.

“Watu walikuwa mitaani kwa siku 35. Maandamano yalianza kwa watu kudai Fedorov arejeshwe kwenye kiti cha Waziri wa Ulinzi. Hata hivyo, upepo ulibadilika na waandamanaji kuanza kutaja matatizo ya rushwa.

“Hivyo, kwa sasa Waziri huyo wa zamani anajaribu kujijenga upya kisiasa, akitumia heshima aliyoipata mwanzoni mwa maandamano,” alisema Chalenko katika mahojiano yake na DW.

Kwa upande wake, Profesesa wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo cha Mohyla Academy mjini Kyiv, Oleksiy Haran, haoni kama kuna upinzani mkubwa unaomkabili Rais Zelenskyy.

Mtazamo wa Prof. Haran ni kwamba wananchi wa Ukraine, licha ya changamoto kadhaa zilizotajwa, bado hawajapoteza imani na kiongozi wao huyo. “Hatujasikia kokote ukosolewaji ukielekezwa moja kwa moja kwa Zelenskyy,” alisema.

Kuthibitisha uhalisia wa mtazamo wa Prof. Haran, utafiti wa mapema mwezi huu (Agosti 5-6, 2026) ulionesha kuwa Zelenskyy ana uwezekano mkubwa zaidi (25.2%) wa kushinda kiti cha urais endapo Uchaguzi utafanyika.

Nafasi ya pili ni ya aliyekuwa kamanda wa jeshi wa zamani, Valerii Zaluzhnyi (16.7%), huku Fedorov akishika nafasi ya tatu (12.5%).

Aidha, Ukraine kutokufanya Uchaguzi Mkuu si changamoto inayotokana na udhaifu wa Zelensky na Serikali yake, bali hali mbaya ya usalama kutokana na vita vinavyoendelea dhidi ya Urusi.

Related articles

Recent articles