22.5 C
New York

Chuki dhidi ya wageni; ‘Wasauzi’ wanawafundisha nini viongozi Afrika?

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

RAIA wa kigeni zaidi ya 17,600 wameondoka Afrika Kusini tangu Aprili, 2026 kutokana na vurugu walizofanyiwa na wenyeji wao. ‘Wasauzi’ hawataki wageni ‘wanaozamia’ katika nchi yao.

Ukifuatilia zaidi, chuki hizo zinatokana na jambo moja tu. Waafrika Kusini, hasa vijana, wanahisi ugumu wa maisha walionao huko mitaani unatokana na wingi wa wageni.

Kwamba wageni wanachukua nafasi zao za kazi. Wageni wanasababisha ubora wa huduma za kijamii kupungua. Kwa ufupi, wageni wanasababisha ‘vyuma vikaze’.

Waafrika Kusini wanapoitazama nchi yao, wanaiona imepiga hatua kubwa ya kiuchumi. Imejengeka kama au kuliko hata baadhi ya nchi za Ulaya. Wanahisi wanastahili kuishi ‘kibosi’ lakini wageni ‘wanazingua’.

Kielelezo cha Afrika Kusini kuwa kwenye hadhi hiyo ni pale ilipoandaa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010. FIFA walijiridhisha kuwa ni nchi yenye hadhi ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

Turudi kwenye mada. Waafrika Kusini wasisahau mapema, kwamba nchi za Afrika zilizokuwa nao bega kwa bega wakati wa sera ya ubaguzi wa rangi nchini kwao na hatimaye ukapatikana uhuru mwaka 1994.

Hata hivyo, kwa upande mwingine, chuki dhidi ya wageni ni somo kwa serikali za Afrika. Kwa makusudi, zinapaswa kuzigeuza nchi zao kuwa ‘pepo’ kwa raia wake. Kivipi?

Ukifuatilia kwa karibu, sehemu kubwa ya raia wa kigeni wanaokimbilia Afrika Kusini wanavutiwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi, ambayo hawayaoni huko wanakotoka.

Kwa walio wengi, kuishi Afrika Kusini ni asilimia 80 ya kutimiza ndoto za kupata maisha mazuri, wakilinganisha na hali iliyopo katika nchi zao. Wengi wamezikatia tamaa nchi zao na hawazioni zikiwapa uwezekano wa ‘kutoboa’.

Nasisitiza; hili ni somo kwa viongozi wa nchi nyingi za Afrika. Badala ya kuelekeza lawama nyingi kwa Wasauzi, ni wakati wa kuzijenga nchi zao ili nazo ziwe na ushawishi wa kuwabakiza raia wake nyumbani.

Afrika Kusini inaweza kuwa imetangulia lakini haiondoshi ukweli kwamba nchi zote za Afrika zina utajiri mkubwa wa rasilimali. Kila moja ina upekee wake katika utajiri huo.

Kama moja inaongoza kwa madini, basi nyingine itakuwa kinara wa utalii. Na hata madini, basi pia kutakuwa na upekee; moja inaweza kuwa inazalisha dhahabu kwa wingi, na nyingine itaongoza kwa shaba au almasi.

Kwa ufupi, ni nadra na huenda haipo kabisa nchi iliyokosa utajiri wake. Lakini je, utajiri huo unatumika katika kuboresha maisha ya watu au unanufaisha kikundi cha ‘wajanja’ wachache? Viongozi walioko madarakani wana dhamira ya dhati ya kuwainua watu wao?

Kinyume cha majibu sahihi ya maswali hayo, raia wa nchi hiyo hawatofurahia maisha ya nyumbani na badala yake wataendelea kukimbilia Afrika Kusini wakiamini ndiko iliko ‘pepo’.

Related articles

Recent articles