Na Hassan Mwasha, Gazetini
HOJA ya maridhiano ina umuhimu mkubwa. Ukweli ulio wazi ni kwamba nchi ipo kwenye mkwamo unaohitaji meza ya mazungumzo. Tuzungumze kweli kweli.
Si tu tuzungumze, bali pia tuulizane maswali, tupate majibu, tufanye tafakuri, na kisha tuamue kama ni kusameheana au kuwajibishana. Kukaa mezani hakuepukiki.
Kama yaliyopotea ni maisha ya watu, basi mambo hayawezi kupita hivi hivi, kana kwamba waliokufa ni kuku, njiwa, bundi, kasuku au tetere. Hayakuwa maisha ya ndege. Ni binadamu.
Hivyo, hoja ya maridhiano inabeba uzito wa pekee na inapaswa kupewa kipaumbele kuliko mambo mengine yote yanayoweza kuonekana makubwa na muhimu.
Hata hivyo, wasiwasi wangu ni kwamba hoja ya maridhiano kwa sasa haipo tena mikononi mwa wananachi, licha ya kwamba wao ndiyo walioumizwa zaidi na kilichotokea Oktoba 29, 2025.
Wao ndiyo waliopoteza wazazi, watoto, ndugu, jamaa na marafiki, achilia mbali biashara zao kuharibiwa, lakini kwa ninachokiona mpaka sasa, wamepewa ‘siti ya nyuma’ kwenye gari linaloelekea kwenye maridhiano.
Kwa lugha nyingine, wamebaki kuwa watazamaji kwenye mchezo unaohitaji uwepo wao uwanjani, wakiwaacha wanasiasa wakitawala kwa kadiri wanavyotaka au kujisikia.
Tujiulize; msingi wa maridhiano ni upi? Kama ni kuliponya Taifa kwa kile kilochojiri Oktoba 29 na siku chache zilizofuata, iweje wanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na upinzani waubebe na kuuona mjadala huo ni mali yao?
Kwamba ili yawe ni ‘maridhiano sahihi’, basi pande mbili hizo zikae mezani, ziafikiane katika masuala fulani, kisha ziamue kama ni kusamehana au kuadabishana.
Vipi kwa wananchi waliopoteza ndugu na mali zao? Tujiulize; ni kikao kipi walichokaa CCM au wapinzani na wananchi na kupewa dhima hiyo ya kuwabebea wananchi machungu ya Oktoba 29?
Kama hakuna kikao au makubaliano yoyote na wananchi, maridhiano yoyote yatakayofanyika yatakuwa yamebeba sura ya siasa. Kwa maana nyingine, hayo hayatokuwa maridhiano yenye msingi wa kuwaponya wananchi kwa madhila waliyopitia.
Binafsi, sipingani na jitihada kubwa zinazofanywa na CCM, vyama vya upinzani na Serikali katika kupata meza ya maridhiano. Wasisi wangu ni kwamba wananchi wamebaki nyuma, wakiachwa kusubiri kile kitakachoamuliwa na pande hizo ilihali wao ndiyo walioionja joto ya jiwe Oktoba 29.
Naomba kuwasilisha …


