LUSAKA, Zambia
KIONGOZI wa siasa za upinzani nchini Zambia kupitia Chama cha National Reconciliation Party for Unity, Brian Mundubile, ameyapinga matokeo yaliyomrejesha madarakani Rais Hakainde Hichilema.
Katika matokeo yaliyotangazwa na Tume, Mundubile ameshika nafasi ya pili kwa asilimia 38 ya kura, akiachwa mbali na Hichilema aliyeshinda muhula wake wa pili kwa asilimia 60.
Huku baadhi ya wanasiasa wa upinzani wakikamatwa na vyombo vya dola, achilia mbali kuuawa kwa Waziri wa zamani, Mutotwe Kafwaya, taarifa zinaeleza kuwa Mundubile alilazimika kukimbilia mafichoni baada ya kupokea jumbe za kutishiwa maisha.
Hayo yote yanatokea wakati Rais Hichilema akijiandaa kuapishwa katika sherehe zinazotarajiwa kufanyika Septemba 1, 2026 mjini Lusaka, Zambia.
Vyombo vya habari vya Zambia viliripoti kufungwa kwa mahakama zote nchini humo, ikiwamo Mahakama Kuu mjini Lusaka, kwa kile kilichoitwa na mamlaka kuwa ni sababu ya kiusalama.
Kwa upande wake, Chama cha Wanasheria cha Zambia (LAZ) kilidai kuwa kufungwa huko kwa mahakama kulilenga kumzuia Mundubile kufungua kesi ya kupinga matokeo ya urais.
“Kufungwa kwa mahakama ni kuzuia upatikanaji wa haki, hasa kwa mtu anayehitaji msaada wa haraka kutoka kwa mahakama,” ilieleza taarifa ya LAZ na kuongeza:
“Hali hiyo inadhihirisha nia ya mamlaka kuchelewesha kesi ya kupinga matokeo inayopaswa kufunguliwa ndani ya siku saba baada ya mshindi kutangazwa.”
Licha ya ofisi za mahakama kufungwa, maandalizi ya Hichilema kuapishwa yameendelea, ikiwamo Wizara ya Vijana na Michezo kutuma mwaliko kwa waandishi wa habari kuhudhuria sherehe hizo zitakazofanyika katika Uwanja wa Taifa.
Kwa upande mwingine, taasisi za haki za binadamu na LAZ vimeomba kufanyika kwa uchunguzi huru juu ya kamatakamata ya vijana, pamoja na kifo cha Waziri Mstaafu, Kafwaya.
Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International limeeleza kifo cha Kafwaya kuwa ni ujumbe wa hatari kwa demokrasia nchini Zambia, pia likiomba uchunguzi kufanyika.
Hata kabla ya kutangazwa kwa matokeo, tayari wanaharakati na jumuhiya za kimataifa zilisharipoti kuwapo kwa viashiria vya ‘uchafuzi’ katika Uchaguzi huo wa Agosti 13, 2026.
Mathalan, wanaharakati walieleza kukosekana kwa uhuru wa utendaji kazi wa Tume ya Uchaguzi na vyombo vya habari nchini humo. Kwamba pande mbili hizo zilisimama upande mmoja wa Hichilema.
Pia, ujumbe wa Umoja wa Ulaya (EU) ulikosoa mazingira magumu ya upinzani, pia ikieleza kutovutiwa na wingi wa vyombo vya dola, hasa wanajeshi, katika vituo vya upigaji wa kura.


