23 C
New York

Guardiola ameondoka na Man City yake?

Published:

MANCHESTER, Uingereza

BAADA ya filimbi ya mwisho katika mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal jana Agosti 16, 2026, kocha Enzo Maresca alisema bado mapema, hivyo mashabiki wa Manchester City hawapaswi kuwa na wasiwasi. Walifungwa mabao 3-0.

Ni kweli ilikuwa mechi ya kwanza ya ushindani kwa Maresca akiwa kocha wa Man City lakini matokeo hayo yameibua sintofahamu juu ya hatima ya timu hiyo bila kocha Pep Guardiola.

Kilichowashitua mashabiki wa Man City ni kuona timu yao ikiruhusu mawili kabla ya dakika 30 za kipindi cha kwanza cha mechi hiyo iliyochezwa mjini Cardiff, Wales.

Hata ndani ya uwanja, Arsenal ilionekana bora zaidi, ikilinganishwa na Man City isiyo na Guardiola kwenye benchi la ufundi. “Pengo lilikuwa kubwa na la wazi kabisa,” amesema beki wa zamani wa Arsenal, Martin Keown.

Akichambua mchezo huo kupitia kituo cha televisheni cha TNT Sports, Keown alisema: “Arsenal ilishika kila idara, wakati Man City ikionekana haina uhai … Man City ina changamoto nyingi.”

Hoja hiyo ya Keown iliungwa mkono pia na mkongwe wa soka la Scotland, Ally McCoist, akisema: “Man City imepewa darasa. Najua bado mapema lakini ina mengi ya kufanyia kazi.”

Kipindi hiki cha usajili wa kiangazi m, Man City imesajili mchezaji mmoja pekee wa kikosi cha kwanza. Kiungo raia wa England, Elliot Anderson.

Wakati huo huo, imewapoteza Bernardo Silva, John Stones, Manuel Akanji, Nathan Ake, James Trafford, na Rodri aliyetimkia Barcelona.

Je, Arsenal ya kocha Mikel Arteta inakwenda kunyakua tena ubingwa wa Ligi Kuu ya England (EPL), ikizingatiwa kuwa mshindani wake mkubwa, Man City, yuko hoi?

Historia haiipi Arsenal nafasi ya moja kwa moja. Tangu Ligi ilipoanza msimu wa 1992-93, ni timu nane pekee zilizotwaa ubingwa baada ya kubeba taji la Ngao ya Jamii. Kwa hivi karibuni, Man City walifanya hivyo msimu wa 2018-19.

Hivyo, lolote linaweza kutokea. Arsenal wanaingia msimu huu wa 2026-27 wakiwa wameimarisha kikosi. Leandro Trossard, Jakub Kiwior na Christian Norgaard ni wachezaji pekee waliouzwa.

Wakati huo huo, Arteta amewanasa Bruno Guimaraes na Christos Tzolis, pia akimsajili moja kwa moja Piero Hincapie aliyecheza kwa mkopo msimu uliopita (2025-26).

Licha ya kwamba bado ni mapema, usajili wa Tzolis umeanza kulipa baada ya nyota huyo kutoa ‘asisti’ mbili katika mchezo wao dhidi ya Man City. Guimaraes naye aliongeza ubora mkubwa kwenye eneo la kiungo.

Wakati huu Man City ikionekana kupotea, pia Arsenal inaweza isiwe na wasiwasi na timu zingine kubwa msimu huu wa Ligi. Kwanini?

Ukiacha Arsenal, vigogo wote wana makocha wapya. Andoni Iraola ni mpya kwenye benchi la ufundi la Liverpool, kama ilivyo kwa Xabi Alonso (Chelsea), Michael Carrick (Man United), na Roberto de Zerbi (Tottenham).

Ni kutokana na utulivu uliopo kwenye benchi la ufundi, mtandao wa takwimu wa Opta unaipa Arsenal nafasi kubwa (33%) ya kutetea ubingwa wao wa msimu uliopita.

Je, ni rahisi kiasi hicho? Kwa mujibu wa historia, Washika Bunduki hao wa Kaskazini mwa London hawajawahi kutetea taji la Ligi tangu walipofanya hivyo msimu wa 1934-35.

Related articles

Recent articles