Na mwandishi wetu, Gazetini
MWAKA 1932, wakati huo Idi Amin akiwa na umri wa miaka minne, kaka na dada yake walifariki. Ni kipindi hicho pia, wazazi wake waliachana.
Vyanzo mbalimbali vinadai kuwa sababu ya Nyariba (baba yake Idi Amin) kuachana na bi. Aate ni utata wa nani baba halisi wa Idi kati yake na Mfalme Daudi Chwa II.
Baada ya wazazi kuachana, baadhi ya vyanzo vya kihistoria vinaeleza kuwa Idi Amin alikwenda kuishi na ndugu wa mama yake mjini Mawale Parish, Wilaya ya Luweero, Kaskazini-Magharini mwa Uganda.
Akiwa huko, Idi Amin alifanya kazi za uchungaji wa mbuzi akiwa na umri wa miaka nane hadi 10. Katika umri wake mdogo huo, alihamia kwenye nyumba ya Sheikh Ahmed Hussein mjini Semuto na hapo akajifunza usomaji wa Quran.
Mwaka 1940, Idi Amin alihamia mjini Bombo, ambako huko alikwenda kuishi kwa mjomba wake, Yusuf Tanaboo. Alifanya vizuri na kutwaa tuzo mbalimbali za usomaji wa Quran akiwa huko.
Baadaye, Idi Amin na vijana wengine 15 walikamatwa ili kuingizwa kwenye jeshi la kikoloni (Uingereza) nchini Uganda lakini aliachiwa kutokana na umri wake mdogo.
Wakati huo akiwa bado hajafanikiwa hata kuanza shule ya msingi, alihamia Kampala na kufanya kazi mbalimbali za kipato duni, ikiwamo usafi katika Hoteli ya Grand Imperial.
Mwaka 1946, Idi Amin alijiunga na jeshi la kikoloni la King’s African Rifles akihudumu katika eneo la upishi, wakati huo huo akipewa mafunzo ya kijeshi.
Mwaka mmoja tu baadaye, alihamishiwa Kenya, kisha kuwa sehemu ya kikosi kilichopigana na waasi wa Somalia huko Kaskazini mwa nchini humo.
Kufikia mwaka 1959, tayari Idi Amin alishapanda vyeo na kuwa ‘Warrant Officer’, ambacho kwa wakati huo kilikuwa ndicho cheo kikubwa zaidi kwa mtu mweusi ndani ya jeshi la kikoloni la King’s African Rifles.
Wakati wote huo wa utumishi wake jeshini, Idi Amin alikuwa pia mwanamichezo, ambapo alikuwa bingwa wa ngumi za uzito wa juu wa Uganda kuanzia mwaka 1951 hadi 1960. Pia, alikuwa mwogeleaji na mchezaji wa rugby.
Aliporejea Uganda mwaka huo, Idi Amin akawa mkubwa kwenye jeshi na hata kukabidhiwa operesheni ya kumaliza mgogoro mkali kati ya wafugaji wa jamii ya Karamojong (Uganda) na majirani zao wa Turkana (Kenya).
Mtafiti Holger Bernt Hansen anasema mwonekano, tabia, mikakati yake ya mawasiliano, na uzoefu wake ndani ya jeshi la kikoloni, vilimfanya Idi Amin kuwa na ushawishi mkubwa katika maeneo mengi nchini Uganda.
Baada ya Uganda kupata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1962, Idi Amin alipanda cheo na kuwa Kapteni, kisha Meja wa jeshi, kabla ya kuwa Mkuu wa majeshi mwaka 1970.
Ni wakati ambao sasa Uganda ilikuwa chini ya Waziri Mkuu, Milton Obote. Akimtumia Idi Amin kama Mkuu wa vyombo vya dola, Obote alifanya mabadiliko ya Katiba ya kutokutambua urais wa Kabaka Mutesa II, kisha akajitangaza kuwa Rais mpya wa Uganda.
Usikose sehemu ya tatu ya mfululizo wa simulizi hii … Tembelea www.gazetini.co.tz


