Na mwandishi wetu, Gazetini
SUPASTAA wa muziki wa R&B nchini Marekani, Trey Songz, alikuwa katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama jijini Dar es Salaam jana Agosti 14, 2026.
Alialikwa katika Tamasha la IMBEJU Sauti Moja na hii inakuwa mara ya kwanza kwa mwanamuziki huyo kutua katika ardhi ya Tanzania.
Kwa wasiomfahamu, mshikaji huyo ana albamu nane na miongoni mwa ngoma zake zinazokubalika ni ‘Back Home’, ‘Circles’, ‘Can’t Help but Wait’, ‘Say Aah’, na ‘Slow Motion’.
ALIKOTOKEA
Trey Songz, ambaye jina lake halisi ni Tremaine Aldon Neverson, alizaliwa Novemba 28, 1984, huko Petersburg, Virginia. Alianza kuonesha kipaji chake cha kuimba akiwa na umri wa miaka 14 tu.
Hata hivyo, jina lake lilianza kusogea mwaka 2003 baada ya prodyuza Troy Taylor kumkubali na kumsaini kwenye Lebo yake ya muziki ya Songbook Entertainment.
Akiwa hapo, alipata mafanikio makubwa zaidi kupitia albamu yake ya kwanza iitwayo ‘I Gotta Make It’ aliyoachia mwaka 2005. Albamu iliyoingia kwenye Top 20 kwenye chati za Billboard 200 na kuuza nakala zaidi ya 400,000 nchini Marekani.
Mbali ya hiyo, albamu zilizofuta na kuendelea kumuweka vizuri sokoni ni ‘Trey Day’ (2007), ‘Ready’ (2009), ‘Passion, Pain & Pleasure’ (2010), ‘Chapter V’ (2012), ‘Trigga’ (2014), ‘Tremaine’ (2017), na ‘Back Home’ (2020).
KESI ZA WANAWAKE
Anazo nyingi tu. Januari, 22, 2027, mwigizaji wa kike, Keke Palmer, alimfungulia mashitaka kwa kumrekodi kwa siri, kisha kutumia kipande hicho cha video kwenye ‘remix’ ya wimbo wake uitwao ‘Pick Up the Phone’.
Mwaka 2020, mwanamke mwingine alifungua mashitaka akidai Songz alimfanyia unyanyasaji wa kingono katika klabu moja ya usiku mjini Miami, alitaka kulipwa fidia ya Dola milioni 10. Songz alikana mashitaka hayo.
Desemba 30, 2021, staa wa zamani wa moja ya timu za kikapu za wanawake alitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuandika ‘Trey Songz ni mbakaji’.
Kwa mujibu wake, alibakwa na Songz walipokuwa katika chumba cha moja ya hoteli maarufu mjini Las Vegas. Songz alikana na kushinda kesi hiyo.
Februari, 2022, mwanamke mwingine aliibuka na kusema Songz alimbaka mwaka 2016. Kesi hiyo iliondoshwa mahakamani mwaka 2024 baada ya pande mbili kukubaliana.
Mwaka uliofuata, mwanaume aitwaye Tyrelle Dunn, ambaye ni ofisa wa polisi, alidai Songz amemdhalilisha mkewe jijini Las Vegas.


