LONDON, Uingereza
MABINGWA wa Ligi Kuu ya England (EPL) msimu wa 2025-26, Arsenal, wameimarisha safu yao ya kiungo kwa kumsajili Bruno Guimaraes kutoka Newcastle United, usajili uliogharimu Pauni milioni 75.
Mbrazil huyo amesaini mkataba wa miaka minne, akiungana na Declan Rice, Mikel Merino, Martin Zubimendi na Martin Odegaard katika eneo la kiungo la kikosi cha kocha Mikel Arteta.
Msimu uliopita (2025-26), Guimaraes akiwa Newcastle alicheza dakika 2,455 kutokana na majeraha, akizidiwa na Rice na Zubimendi waliocheza dakika zaidi ya 3,000 kila mmoja.
Hata hivyo, licha ya kucheza dakika chache kuliko wawili hao, aliwazidi kwa idadi ya mabao ya kufunga katika mechi za Ligi. Alifunga tisa, wakati Rice alifunga manne na Zubimendi akaweka matano.
Kati ya mabao tisa hayo, nane alifunga katika uwanja wa nyumbani (St James). Zubimendi alifunga manne akiwa Emirates. Rice alifunga bao moja tu katika mechi za nyumbani.
Kwa upande mwingine, Guimaraes ni mzuri pia katika kupiga mashuti. Msimu huo, alipiga mara 36, huku 23 yakilenga lango la timu pinzani.
Ukija katika eneo la asisti (pasi za mabao), Guimaraes alimaliza msimu akiwa na tano, sawa na Rice, ambapo hata hivyo aliwazidi Merino (3) na Zubimendi (1).
Wakati huo huo, Guimaraes amewazidi viungo walipo Arsenal kwa uwezo wa kucheza mipira ya juu. Msimu uliopita, alicheza mipira ya aina hiyo mara 334, akishinda mara 168.
Zubimendi, nyota wa zamani wa Real Sociedad, licha ya kuwa mchezaji aliyeongoza kwa upande wa Arsenal, alishinda mipira ya juu mara 151.
Pia, ukilinganisha na viungo wote wanne wa Arsenal, Guimaraes ndiye aliyechezewa rafu nyingi msimu uliopita. Rafu 75, tofauti na 55 za viungo wote wa Arsenal.


