23.1 C
New York

Hiki ndicho chanzo cha guvu ya waasi Nigeria?

Published:

LAGOS, Nigeria

KWA miaka mingi sasa, Nigeria imegubikwa na matukio ya uhalifu katika maeneo yake mengi. Watu takribani 3,000 wametekwa kwa kipindi cha mwaka mmoja (2024-2025).
Pia, kwa kipindi hicho, watu zaidi ya 3,500 wamepoteza maisha, kwa mujibu wa takwimu za Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Nigeria.

Matukio ya utekaji shuleni yameshika kasi zaidi, ambapo yamejitokeza mara 26 kati ya Aprili, 2014, na Mei, 2026, kwa mujibu wa Kituo cha Ripoti za Uchunguzi (ICIR).

Wakati huo huo, utekaji wa kushinikiza malipo ili kuachia watu umetajwa kuwa biashara kubwa ya mamilioni ya Dola kwa vikundi vya kigaidi.

Kwa upande mwingine, kukosekana kwa uaminifu ndani ya vyombo vya dola ni moja ya sababu zinazochagiza nguvu kubwa ya vikundi hivyo.

Mathalan, hivi karibuni alikamatwa mwanajeshi aliyebainika kuwa na mtandao wa kuvipa sare za jeshi vikundi vya kigaidi. Mohammed Yusuf alidakwa Kaskazini-Mashariki mwa Mji wa Maiduguri.

Msemaji wa jeshi, Mohammed Goni, alisema mwanajeshi huyo aliwahi kufanya kazi katika kiwanda cha sare za jeshi na alikamatwa akiwa njiani kuelekea mpakani mwa nchi jirani ya Cameroon kwa ajili ya kujificha.

Kwa upande wake, Bashir Galma, ambaye ni mchambuzi wa masuala ya usalama, amesema kwa sasa nchini Nigeria haishitui tena kusikia watumishi wa vyombo vya dola wanashirikiana na wahalifu.

“Najua kuna wakati (jeshi) linakuwa na mpango wa kushambulia eneo fulani lakini taarifa zinawafikia Boko Haram au vikundi vingine kupitia mtandao wao ndani ya jeshi,” amesema mstaafu huyo wa jeshi.

Aidha, madai ya aina hiyo yaliwahi pia kutolewa na Jimbo la Borno, Babagana Zulum, mwaka 2025, akisema ndani ya vyombo vya dola vya Nigeria wapo mashushu wa Boko Haram na vikundi vingine vya kigaidi.

Babagana ambaye Jimbo lake ni miongoni mwa maeneo yenye usalama mdogo, alisema hata baadhi ya wanasiasa wanashirikiana na waasi kwa kuwapa taarifa.

Mwezi mmoja tu baada ya kauli hiyo, wanajeshi watatu walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa makosa ya kushirikiana na waasi.

Kwa upande wake, mchambuzi Galma anaamini malipo kiduchu wanayopata serikalini yanachangia baadhi ya wanajeshi kuingia kwenye mtego wa kushwawishiwa na vikundi hivyo.

Katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), mmoja ya wananchi aliyeachiwa na waasi baada ya familia yake kulipa Dola 42,000, anafichua alivyomuona mwanajeshi akigawana ‘mshiko’ huo na waasi.

“Walitushusha sehemu na kulikuwa na mwanajeshi mmoja ambaye alipeana nao mikono na kucheka,” anasema mwaanchi hiyo kwa sharti la jina lake kuhifadhiwa kwa sababu za kiusalama.

Mwingine ni mkulima anayejitambulisha kwa ni la Yahuza Isa, ambaye alitekwa katika Jimbo la Zamfara. Anauliza: “Mimi tu najua makazi ya waasi. Kwanini (vyombo vya dola) haviendi kuwamaliza?”

Mwingine ambaye hata hivyo alitaka jina lake kuhifadhiwa, anasema alishikiliwa na waasi kwa siku 30 mwishoni mwa mwaka 2024.

Anasema akiwa kwenye kambi ya waasi hao, huku macho yakiwa yamezibwa kwa kitambaa, alisikia mara kadhaa mlio wa helikopta ya jeshi ikiingia eneo hilo.

“Mara ya kwanza niliposikia, nilihisi imekuja kutuokoa, lakini tukasikia inaondoka,” anasema na kusisitiza kuwa helikopta hiyo ilikuja mara kadhaa, hivyo kuamini kuwa waasi wanapata ushirikiano mkubwa kutoka serikalini.

Hata hivyo, Abdullahi Abdullahi, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usalama, anasema hata baadhi ya wananchi wamekuwa wakivujisha taarifa kwa waasi. “Ndiyo maana tatizo limeendelea kuwapo miaka kwa miaka,” amesema.

Related articles

Recent articles