24.4 C
New York

Infantino kung’oka FIFA, nani kuchukua nafasi yake?

Published:

NYON, Uswis

MAMBO hayuko vizuri kwa Rais Gianni Infantino. Ameachana na mpango wake wa kuuza hisa za michuano ya FIFA, ikiwamo Kombe la Dunia, baada ya kukosolewa vikali.

Kwa mtazamo wa wachambuzi wengi wa mchezo wa soka, ni mpango uliomchafua na hata kuiweka pabaya nafasi yake ya kushinda Uchaguzi ujao wa Machi, 2027.

APINGWA KILA KONA

Mpango wa kuziuzia hisa kampuni binafsi katika michuano yote ya FIFA ulipingwa kila kona. Miongoni mwa walioukataa na hata kusema Infantino hafai tena kuliongoza Shirikisho hilo ni Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham.

Pia, Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) nalo liliukataa mpango huo na kutishia wanachama wake kutokushiriki fainali za Kombe la Dunia endapo ungeendelea.

Infantino alipokea pia ukosolewaji kutoka kwa mashirikisho makubwa mawili; Concacaf (Shirikisho la Amerika ya Kaskazini na Kati na Visiwa vya Caribbean) na AFC (Shirikisho la Asia).

Wakati huo huo, Infantino alipata pigo jingine zito baada ya aliyekuwa mshauri wake, Carlos Cordeiro, kutangaza kujiuzulu. Ndiye aliyekuwa mshauri wa Kikosi Kazi cha maandalizi ya Kombe la Dunia mwaka huu (2026).

ANGUKO LAKE NDANI YA FIFA?

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha BBC Sport mapema wiki hii, aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Soka cha Uingereza (FA), David Bernstein, alisema:

“Infantino kutokuungwa mkono katika mpango wake huo ni anguko na ishara ya mlango wa kutokea … Kama bado anakubalika, basi anaweza kuendelea,” alisema Bernstein.

Wakati huo huo, aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa FIFA, Jim Boyce, amesema endapo Infantino atabadilisha haraka upepo mbaya uliopo sasa, bado ana nafasi ya kushinda Uchaguzi ujao na kuendelea kuiongoza FIFA.

“Kama ningekuwa mtu wa ‘kubeti’, ningesema bado ana nafasi ya kushinda miaka mingine minne ya mwisho,” alisema Boyce.

UZOEFU WAKE KAZINI

Infantino mwenye umri wa miaka 56, amekuwa Rais wa FIFA tangu mwaka 2016 baada ya kuwa Katibu Mkuu wa UEFA kwa miaka saba.

Alishinda kiti cha urais wa FIFA akiwa na kura 115 dhidi ya 88 alizopata mpinzani wake, ambaye ni Rais wa sasa wa Shirikisho la Soka la Asia, Sheikh Salman al-Khalifa.

Aliingia madarakani wakati taswira ya FIFA ikiwa imechafuliwa na tuhuma za rushwa zilizosababisha Sepp Blatter kujiuzulu na kufunguliwa mashitaka.

Tangu aingie madarakani, Infantino ameshinda chaguzi mbili bila kupingwa na ilitarajiwa kuwa hivyo pia katika Uchaguzi ujao wa Machi, 2027, kabla ya hiki kilichotokea.

NANI KUCHUKUA NAFASI YAKE?

Kuelekea Uchaguzi wa Machi, 2027, yapo majina kadhaa yanayotajwa na kupewa nafasi kubwa ya kukalia kiti cha Infantino ndani ya FIFA, akiwamo Rais wa Concacaf, Victor Montagliani.

Montagliani ni Rais wa zamani wa Chama cha Soka cha Canada na alihusika vilivyo katika maandalizi ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu zilizoandaliwa na nchi hiyo kwa kushirikiana na Marekani na Mexico.

Rais wa Shirikisho la Soka la Asia, Sheikh Salman bin Ebrahim Al Khalifa, naye anatajwa. Aliingia madarakani mwaka 2013 na atwania muhula wake wa nne mwaka 2027.

Pia, wamo Rais wa PSG ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Soka za Ulaya, Nasser Al-Khelaifi, na Katibu Mkuu wa FIFA, Mattias Grafstrom.

Rais mpya wa FIFA atatangazwa kupitia Mkutano Mkuu wa 77 utakaofanyika Machi, 2027, nchini Morocco. Wagombea wanapaswa kukabidhi majina yao kufikia Novemba 18, 2026.

Related articles

Recent articles