KAMPALA, Uganda
KIONGOZI mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Dk. Kizza Besigye, amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) mjini Kampala baada ya kuanguka na kupoteza fahamu wakati wa kusikilizwa kwa kesi inayomkabili ya uhaini.
Besigye, mwenye umri wa miaka 70, amekuwa kizuizini tangu Novemba 2024. Tukio hilo lilitokea baada ya kupinga uamuzi wa mahakama wa kumteua wakili kutoka upande wa serikali kumwakilisha. Mashahidi waliokuwapo mahakamani walisema alisikika akipaza sauti akisema “wacheni” mara kadhaa kabla ya kuanguka ghafla.
Baada ya tukio hilo, walinzi wa gereza walimkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Mulago. Hata hivyo, familia yake ilipinga apatiwe matibabu na madaktari wa serikali.
Mke wake, Winnie Byanyima, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS), alisema kupitia mtandao wa X kuwa hali ya Besigye ni mbaya.
“Bado amepoteza fahamu. Hawezi kuzungumza na haitikii hata anapopimwa mwitikio wa maumivu,” aliandika Byanyima.
Amesema familia haitaruhusu maafisa wa serikali kushiriki katika matibabu yake na inataka Besigye ahudumiwe na daktari wake binafsi katika hospitali ya kibinafsi.
Ripoti zinaeleza kuwa kitengo cha ICU anacholazwa kimeimarishwa ulinzi, huku dada yake ambaye pia ni daktari wake akiruhusiwa kumwona.
Wakati huo huo, changamoto za kisheria zinaendelea kumkabili Besigye. Wakili wake mkuu, Erias Lukwago, anazuiliwa baada ya kukamatwa mwezi uliopita kwa tuhuma zinazohusiana na kesi hiyo, huku wakili mwingine kutoka Kenya, Martha Karua, akizuiwa kuingia Uganda alipokuwa akielekea kumwakilisha.
Mwana wa Besigye, Adam Ampa, ametoa wito kwa Rais Yoweri Museveni na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kumuachilia baba yake kwa misingi ya kibinadamu kutokana na hali yake ya afya.
Besigye, ambaye amewahi kugombea urais dhidi ya Rais Museveni mara nne, alikamatwa nchini Kenya mwaka 2024 kabla ya kurejeshwa Uganda ambako anakabiliwa na mashtaka ya uhaini.


