Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
JUHUDI za Serikali za kupambana na ndoa za utotoni zimezaa matunda mkoani Shinyanga baada ya operesheni maalumu kumuokoa binti aliyekuwa amefaulu kujiunga na Kidato cha Tano, lakini akawa ameozeshwa kabla ya kuanza masomo.
Operesheni hiyo ilifanyika usiku wa kuamkia Julai 29, 2026 katika Kitongoji cha Majengo, Kijiji na Kata ya Lyamidati, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, binti huyo, ambaye utambulisho wake umefichwa kwa mujibu wa sheria za kulinda watoto, alikuwa ameishi na kijana mmoja kwa takribani miezi miwili baada ya kudaiwa kuozeshwa kwa mahari ya Shilingi milioni 4.5. Familia yake pia ilidaiwa kuwa tayari imekubaliana kupokea mahari hiyo, huku maandalizi ya ndoa yakitarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Agosti.
Baada ya kuhojiwa, binti huyo alikiri kuwa alikuwa akiishi na kijana huyo licha ya kuwa alikuwa amechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule moja wilayani Nzega, mkoani Tabora.
Kwa upande wake, kijana aliyekuwa akiishi naye, Bundala Mashiku, alisema hakufahamu kuwa binti huyo alitakiwa kuendelea na masomo.
“Nilijua amemaliza Kidato cha Nne. Alikuwa nyumbani, sikujua kama alitakiwa kwenda shule, ndiyo maana nikaanza kuishi naye,” amesema Bundala.
Naye baba wa kijana huyo, Mshigu Sylvester, alithibitisha kuwa familia hizo mbili zilikuwa zimekubaliana kuhusu mahari.
“Tulikuwa tumekubaliana mahari ya Shilingi milioni 4.5, na mwanzoni mwa Agosti tulitarajia kupokea Shilingi milioni tatu kama malipo ya awali,” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, alisema operesheni hiyo ni sehemu ya kampeni endelevu ya Serikali ya kutokomeza ndoa za utotoni na kuhakikisha watoto wa kike wanapata haki yao ya elimu.
“Hatutavumilia vitendo vinavyowanyima watoto haki yao ya elimu. Serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaohusika na ndoa za utotoni,” amesema Mtatiro.
Kwa sasa, Bundala Mashiku na Mshigu Sylvester wanashikiliwa na Jeshi la Polisi huku uchunguzi ukiendelea. Serikali imewataka wazazi na walezi kuacha kuwaozesha watoto na badala yake kuwawezesha kuendelea na elimu ili watimize ndoto zao na kuchangia maendeleo ya taifa.


