Na Hassan Mwasha
KAMA ni mfuatiliaji wa tamthilia za Tanzania zinazorushwa kupitia vituo vya televisheni pekee, basi ni wazi unapitwa na mengi. Jiongeze!
Kwa sasa, mtandao wa kijamii wa YouTube umegeuka kambi kubwa ya tamthilia za Bongo, zikiwamo zilizo kwenye mtindo wa mwendelezo (series).
Uwepo wa YouTube umetanua uwanja na kuufanya kuwa mpana kwa waigizaji kujitafutia umaarufu, tofauti na awali ambapo walipaswa kusubiri hadi kazi zao zirushwe kupitia televisheni.
Leo hii, YouTube imezalisha wasanii wengi na tamthilia nyingi zenye majina makubwa katika tasnia ya burudani hapa chini, licha ya kwamba hawakupitia na kwenye vituo vya runinga.
Kwa kuwataja kwa uchache, unaweza kuwagusa Madebe Lidai, Clam Vevo, Chumvi Nyingi, Kicheche OG, Manyanya, Steve Mweusi na Ndaro.
Tofauti na miaka mingi iliyopita, ambapo mwigizaji alihitaji kuonekana kupitia tamthilia ya televisheni ili awe maarufu nchini, sasa picha limegeuka.
Kwamba kwa sasa wengi wanapata ustaa kupitia YouTube, ndipo vituo vya runinga vinapohaha kuwatafuta kwa ajili ya kufanya nao mahojiano (interview).
Kwa upande mwingine, YouTube si tu imetengeneza jukwaa tofauti na fursa nyingine, bali pia imezalisha ushindani kati ya wasanii wake na wale wa tamthilia za vituo vya televisheni.
Kwa namna moja au nyingine, ushindani huo umechangia kwa kiasi kikubwa ubora wa kazi tunaoziona pande zote mbili; kwenye vituo vya televisheni na zile za YouTube.
Mathalan, wakati wapenzi wa tamthilia zinazorushwa kwenye vituo vya runinga wakifurahia ubora wa ‘Kombolela’, huko YouTube kuna ‘Big Boss (Season 2)’.
Zote mbili, si tu uzuri wa stori, bali pia viwango vya juu unaweza kuviona katika uwezo wa waigizaji na uwekezaji mkubwa uliofanyika.
Vilevile, uwepo wa YouTube unaweza kuwa umeondosha ukiritimba waliokuwa wakikumbana nao wasanii, hasa wachanga, mbele ya baadhi ya ‘washika dau’ kwenye vituo vya runinga.
Kupitia YouTube, anachohitaji msanii ni kufungua akaunti yake (bure), kurekodi kazi, kuipandisha, kisha ‘ku-push’ ili iwafikie watazamani wengi.
Hakuna tena haja ya kumlamba miguu mshika dau ili airushe hewani. YouTube imeondosha utumwa wa aina hiyo uliokwaza na huenda hata kuzima vipaji vingi.
Katika sura nyingine, hata waigizaji wa tamthilia zinazorushwa kwenye runinga, pia nao wamekuwa wakitumia YouTube kuposti kazi ili kujiongezea ushawishi.


