29 C
New York

IWPG: Tusikubali vita kuwa jambo la kawaida

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

VIONGOZI wa wanawake kutoka Afrika, Ulaya na maeneo mengine duniani wametoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za kujenga amani duniani, wakisisitiza kuwa vita havipaswi kukubalika kama sehemu ya maisha ya kawaida, huku wakihimiza ushiriki mkubwa wa wanawake katika kutafuta suluhu za migogoro.

Wito huo umetolewa wakati wa Kongamano la Kimataifa la Wanawake kwa Amani lililoandaliwa kwa njia ya mtandao na International Women’s Peace Group (IWPG) kwa siku mbili kuanzia Julai 20, likiwakutanisha wanawake 1,067 kutoka kanda za Asia-Pasifiki, Afrika na Ulaya, Amerika, pamoja na Asia Kusini na Mashariki ya Kati.

Kongamano hilo lilikuwa sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake kwa Amani wa mwaka 2026 utakaofanyika Septemba nchini Korea Kusini, ambapo mapendekezo yatakayokusanywa kutoka kanda mbalimbali yatawasilishwa kama mwongozo wa kimataifa wa kuimarisha amani.

Akifungua kongamano hilo, Rais wa IWPG, Jeon Na-young, alisema suluhu za migogoro haziwezi kupatikana bila kusikiliza sauti za wanawake wanaoishi katika jamii zinazokumbwa na migogoro.

“Wanawake wanaoishi katika jamii hizo wanaelewa changamoto zao kuliko mtu mwingine yeyote. Suluhu za kudumu lazima zitokane pia na uzoefu na hekima zao,” alisema.

Katika mjadala kuhusu hali ya usalama barani Ulaya, Rais wa Heshima wa tawi la Hispania la Women’s International League for Peace and Freedom (WILPF), Carmen Magallón, alionya kuhusu ongezeko la mbio za silaha duniani, akisema hali hiyo inaweza kufanya vita kuonekana jambo la kawaida.

“Vita si jambo la asili, ni uamuzi wa binadamu. Hatupaswi kuruhusu vita vikubalike kama hali ya kawaida,” alisema.

Kutoka Uturuki, Sanem Arikan alisema sanaa na utamaduni vina nafasi muhimu katika kujenga maelewano na kuimarisha mshikamano wa kijamii, akisisitiza kuwa amani huwafikia watu kwa urahisi kupitia lugha ya sanaa.

Wawakilishi kutoka Cameroon walielezea athari za muda mrefu za migogoro kwa wanawake na vijana, wakisisitiza kuwa ushiriki wa wanawake katika kujenga amani ni uwekezaji muhimu kwa maendeleo endelevu.

Mtaalamu wa masuala ya amani kutoka Tume ya Kitaifa ya Umoja na Ushirikiano ya Kenya (NCIC), Regina Mutiru Mwendwa, alisema kurejesha usalama pekee hakutoshi baada ya migogoro, akisisitiza umuhimu wa huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kwa waathirika.

Washiriki kutoka Jamhuri ya Czech na Moldova walieleza kuwa elimu, ujasiriamali, ushirikishwaji wa jamii na kujenga mazingira ya kuaminiana ni msingi muhimu wa amani ya kudumu.

IWPG ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali linaloongozwa na wanawake, linalojihusisha na kuhamasisha amani kupitia elimu, utetezi wa haki, ushirikiano wa kimataifa na kuongeza ushiriki wa wanawake katika juhudi za kuzuia migogoro na kujenga jamii zenye amani.

Related articles

Recent articles