29 C
New York

Netanyahu kukamatwa Marekani, kupelekwa ICC?

Published:

WASHINGTON DC, Marekani

WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, atakuwa Ikulu ya Marekani Jumanne ya wiki ijayo alikoalikwa na mwenyeji wake, Rais Donald Trump.

Netanyahu amealikwa na Rais Trump kwa ajili ya maziko ya Seneta Lindsey Graham, ambaye alikuwa mshirika mkubwa wa Israel. Alifariki ghafla siku chache zilizopita mjini Washington.

“Kwa mwaliko wa Rais Trump, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ataondoka Jumatatu kuelekea Washington kwa mwaliko rasmi,” imeeleza taarifa ya Ofisi ya Netanyahu.

“Katika sehemu ya ziara hiyo, Waziri Mkuu atakutana na Rais Trump Ikulu ya Marekani Jumanne na kuhudhuria maziko ya Seneta Lindsey Graham.”

Hiyo itakuwa ziara ya saba ya Netanyahu, akiwa kiongozi peke duniani aliyefika mara nyingi katika Ikulu ya Marekani tangu Rais Trump aliporejea madarakani.

Hata hivyo, ziara ya safari hii inakuja wakati Marekani ikiwa kwenye mapambano makali dhidi ya Iran baada ya makubaliano ya kusitisha vita kukiukwa na pande zote mbili.

Israel, kwa upande wake, haikuwa muumini wa mkataba wa usitishaji vita ulioingiwa na Marekani na Iran wiki chache zilizopita.

Wakati huo huo, Israel nayo iko kwenye uwanja wa vita nchini Lebanon. Marekani nayo haivutiwi na hatua ya Israel kukataa kuondosha wanajeshi wake Kusini mwa Taifa hilo la Mashariki ya Kati.

Kwa pamoja, tofauti hizo zinaelezwa na wachambuzi wa siasa kutishia uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Marekani na Israel.

Wakati huo huo, Israel iko kwenye kitanzi cha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ikishutumiwa kwa uhalifu wa kivita na dhidi ya binadamu katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa takwimu za mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN), watu milioni 1.4, sawa na asilimia 67 ya wakazi wa Gaza, wengi wao wakiwa ni Wapalestina, wanakabiliwa na janga la njaa.

Kwa upande mwingine, mashambulizi ya Israel yamesababisha Wapalestina takribani 73,311 kupoteza maisha, wakiwamo 86 tangu kuanza kwa mwaka 2026.

Kutokana na kadhia hizo na zingine, ikiwamo maelfu ya raia wa Palestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya Israel pasi na kufunguliwa mashitaka, ICC imeituhumu Israel kwa uhalifu wa kivita na ilitoa kibali cha Netanyahu kukamatwa.

Hivi karibuni, Meya wa New York, Zohran Mamdani, alikoleza moto katika jambo hilo, akizitaka mamlaka za Marekani kumkamata Netanyahu na kumkabidhi ICC.

Awali, Mamdani aliwahi kutishia kutumia polisi wa New York kumkamata Netanyahu, kabla ya kuibuka baadaye na kusema hana mamlaka hayo.

Ukiacha ziara ya sasa, Netanyahu atakuwa New York City kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ifikapo Septemba, 2026.

Hata hivyo, Marekani si sehemu ya ICC, hivyo haiwajibiki moja kwa moja kumkamata Netanyahu au kiongozi mwingine anayeshitakiwa na Mahakama hiyo.

Vilevile, Rais Trump amekuwa mkosoaji mkubwa wa ICC, akienda mbali zaidi na kuwawekea kikwazo cha kuingia nchini humo baadhi ya maofisa wake.

Kuelekea ziara ya Netanyahu, Rais Trump ameshaweka wazi kuwa Waziri Mkuu huyo hatokamatwa kwa njia yoyote akiwa katika ardhi ya Marekani.

“Benjamin Netanyahu hatokamatwa kwa staili yoyote ile akiwa Marekani,” aliandika Rais huyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Truth Social.

Hata hivyo, Netanyahu ameibua hisia mseto kwa baadhi ya wanasiasa wa Marekani, wakiwamo wa Chama cha Republican cha Rais Trump.

Kwa walio wengi, Israel imeiingiza Marekani katika vita dhidi ya Iran, ambavyo kimsingi havina masilahi yoyote ya kisiasa wala kiuchumi kwa Marekani.

Related articles

Recent articles