24.9 C
New York

Vijana na tatizo la ajira duniani

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

TATIZO la ajira kwa vijana limeendelea kuzalisha maandamano katika nchi mbalimbali duniani, safari hii India ikichukua nafasi.

Hamasa ya vijana wa Chama cha Vijana cha Cockroach (CJP) ilianzia mitandaoni, kabla ya kuingia barabarani na kusababisha vurugu zilizojeruhi baadhi ya polisi.

Ni kama ambavyo imeshuhudiwa kwa nyakati tofauti katika nchi za Afrika Kusini na Morocco.

Aidha, ni kama ilivyotokea mwaka 2025 katika nchi za Kenya, Peru, Nepal, Indonesia, chanzo kikiwa ni kile kile, uhaba wa ajira kwa vijana.

Hasira za vijana dhidi ya serikali zao zinakuja wakati huu idadi ya wahitimu wa elimu ya juu ikiendelea kuongezeka katika nchi nyingi duniani.

Wakati huo huo, nafasi chache za ajira zilizokuwepo zimeminywa zaidi na kasi ya teknolojia ya akili-unde (AI).

Tatizo hilo la uhaba wa ajira kwa vijana limeonekana hata katika nchi zilizoendelea kiuchumi duniani, ikiwamo China.

Katika Taifa hilo la Asia, vijana wa umri kati ya miaka 15 na 24 wanatajwa kuwa wahanga wakubwa wa ufinyu wa fursa ajira aidha kwa kukosa uzoefu au ‘koneksheni’.

Serikali nayo inatupiwa lawama kwa kasi ndogo ya uzalishaji wa ajira isiyoendana na idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu.

Kufikia Mei, 2026, asilimia 15.6 ya vijana wenye umri wa miaka 16 hadi 24 wanaoishi katika maeneo ya mijini waliripotiwa kuwa nje ya soko la ajira, kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya China.

Hali ni mbaya pia kwa Uingereza, moja ya mataifa makubwa kiuchumi. Idadi ya ajira mpya kwa wahitimu wa vyuo vikuu imeshuka, ikilinganishwa na zile za watu wa kawaida.

“Kwa Uingereza, ajira mpya zinazotangazwa kwa ajili ya wahitimu imeshuka … Nyingi zinafanywa na AI,” anasema Golo Henseke, mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha London.

Mbali na Uingereza, idadi ya vijana walioajiriwa au walio kwenye vituo vya mafunzo imeshuka kwa kiasi kikubwa barani Ulaya.

Hilo limeshuhudiwa zaidi katika mataifa ya Austria na Ujerumani. “Ukosefu wa ajira kwa vijana siyo jambo jipya tena Ulaya,” anasema Henseke.

Aidha, katika ripoti yake, Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) linaeleza kuwa hata vijana wenye sifa bado hawana ajira katika nchi za Latin Amerika, Kusini mwa Asia, na Kusini mwa Afrika.

ILO ilibaini kuwa kati ya 2023 na 2025, kiwango cha vijana wasio na ajira iliongezeka katika nchi nane kati ya Mashariki ya Asia, Amerika ya Kaskazini (Marekani na Canada), Kusini-Mashariki mwa Asia na Pacific.

Hata hivyo, katika taarifa yake, ILO imeeleza kuwa taaluma kubwa kama sayansi, uhandisi, afya na taarifa na mawasiliano, zinafanya vizuri katika mataifa mengi.

Related articles

Recent articles