LONDON, Uingereza
SHIRIKISHO la Soka la Italia (FIGC) limeanza mazungumzo na kocha aliyeondoka Manchester City, Pep Guardiola, likijaribu kumshawishi kuchukua nafasi ya Gennaro Gattuso aliyeondoka kwenye benchi la ufundi la timu ya taifa.
Gattuso aliachia ngazi Aprili, 2026, baada ya Italia kufungwa na Bosnia katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia.
Ripoti kutoka Italia zinaeleza kuwa Mkurugenzi wa Ufundi, Paolo Maldini, ameongozana na mshauri wake, Leonardo, kwenda Hispania kukutana na Guardiola.
Endapo Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 55 atapewa kazi, atakuwa kocha wa pili wa kigeni kuwahi kuinoa timu ya soka ya Taifa ya Italia.
Je, atawapiku wakongwe wa soka la Italia, Roberto Mancini na Andrea Pirlo, ambao pia wanahusishwa na kibarua hicho?
Guardiola, kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Hispania, amekuwa nje ya kazi tangu alipoondoka Man City aliyoinoa kwa miaka 10 na hii itakuwa mara yake ya kwanza kufanya kazi na timu ya taifa.
Ni mzungumzaji mzuri wa Kiitaliano, lugha aliyojifunza kwa misimu miwili aliyocheza Serie A (2001 – 2003) akiwa na klabu za Brescia na AS Roma.
‘Azzurri’ imekuwa hoi tangu ilipotwaa ubingwa wa EURO 2021, ambapo haijafuzu Kombe la Dunia kwa misimu mitatu mfululizo (2018, 2022 na 2026).
Kabla ya anguko hilo, Italia ilikuwa moja ya mataifa yenye ufalme wake mkubwa katika soka la kimataifa, ikitwaa mara nne ubingwa wa Kombe la Dunia na mara mbili taji la EURO.
Endapo Guardiola ataajiriwa, mtihani wake wa kwanza utaanzia kwenye michuano ya Nations League, ambapo Italia itaivaa Ubelgiji (Septemba 25, 2026) mjini Roma.
Baada ya hapo, utafuata mtihani wa kuwania tiketi ya kushiriki fainali za EURO za mwaka 2028, michuano itakayofanyika katika nchi mbili za Uingereza na Jamhuri ya Ireland.


