TORONTO, Canada
WIKIENDI hii, Julai 5, 2026, itashuhudiwa mechi kali ya hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia kati ya Brazil na Norway ya straika Erling Haaland.
Norway ilivuka hatua ya 32 Bora kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ivory Coast, wakati Brazil walipata kama huo mbele ya Japan.
Hivyo, Brazil na Norway zitakwaana Julai 5, 2026 kwa mchezo wa jijini New York, Marekani, utakaoamua timu ya kwenda robo fainali.
Straika wa Norway, Erling Haaland, ambaye tayari ana mabao matano, amesema si mechi rahisi kwao na wana nafasi finyu ya kuifunga Brazil.
Hata hivyo, licha ya Haaland na wengi kuipa Brazil nafasi kubwa ya kuifunga Norway, rekodi zimegoma.
Brazil haijawahi kuondoka na ushindi katika mechi yoyote kati ya nne ilizowahi kukutana na Norway.
Mechi ya kwanza ilikuwa ya kirafiki na ilichezwa Julai, 1988 nchini Norway na ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mei, 1997, timu hizo zilikutana tena kwa mechi ya kirafiki na safari hii Norway wakiwa nyumbani waliitandika Brazil mabao 4-2.
Mchezo wa tatu ulichezwa Juni, 1998 na ulikuwa wa Kombe la Dunia. Brazil iliteseka tena kwa kichapo cha mabao 2-1.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kuvaana ilikuwa Agosti, 2006. Ulikuwa mchezo wa kirafiki na dakika zake 90 zilitamatika kwa sare ya bao 1-1.


