Na mwandishi wetu, Gazetini
MWISHONI mwa mwaka 2025, Madagascar ilitikiswa na maandamano makubwa ya vijana wa Gen-Z walioingia barabarani wakipinga hali mbaya ya kiuchumi, wakati huo wakishuhudia Serikali yao ikitawaliwa na vitendo vau rushwa.
Mbali na mengine juu ya mdororo wa huduma za kijamii, pia vijana walieleza kuchoshwa na changamoto ya uhaba wa maji na umeme.
Maandamano yaliyosababisha vifo vya raia 22 na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa yalishinikiza Rais Andry Rajoelina kujiuzulu na hatimaye kiongozi huyo na wenzake serikalini kukimbilia nje ya nchi.
Baadaye, jeshi la nchi hiyo chini ya Kanali Michael Randrianirina liliingia madarakani kwa ahadi ya kuongoza hadi utakaofanyika Uchaguzi Mkuu ifikapo mwaka 2027.
Tangu uongozi wa kijeshi uingie madarakani, siasa za nchi hiyo zimeonekana kujenga ushirikiano mkubwa na kidiplomasia na Taifa la Urusi.
Itakumbukwa, Rais wa Bunge la Madagascar, Siteny Randrianasoloniaiko, alikuwa mjini Moscow kwa siku tano, kuanzia Novemba 5-10, 2025, kwa lengo la kuimarisha mahusiano.
Desemba, 2025, ziliibuka taarifa kuwa ujumbe wa viongozi wa kijeshi takribani 40 kutoka Urusi ukiongozwa na Jenerali Andrei Averianov uliingia kwa siri nchini Madagascar.
Matokeo ya ziara hiyo ya siri ni kile kilichotokea Februari, 2026, ambapo Urusi iliipatia Madagascar helikopta na mashine zingine nzito za kivita.
Kama hiyo haitoshi, Aprili Mosi, 2026, Madagascar ilipokea magari ya kivita, silaha, mabomu na sare za jeshi kutoka Urusi.
Hata hivyo, uhusiano kati ya mataifa hayo una historia ndefu, tangu wakati wa Vita Baridi, ambapo baada ya kuanguka kwa Serikali mwaka 1972, viongozi wa kijeshi nchini Madagascar walianza mahusiano na Umoja wa Kisoviet.
Mwaka 1975, kikiwa chini ya Rais Didier Ratsiraka wakati huo, Kisiwa cha Madagascar kilitambulisha rasmi mfumo wa ujamaa.
Ni kuanzia hapo, Madagascar ikawa inapokea misaada mingi kutoka Umoja wa Kisoviet, ikiwamo mafunzo ya kijeshi, silaha, na kujengewa viwanda vya unga na saruji.
Katika eneo la elimu, pia Madagascar iliweza kunufaika, ambapo Umoja wa Kisoviet uliwapatia maelfu ya vijana wa nchi hiyo ufadhili wa masomo ya elimu ya juu.
Hadi leo hii, vijana wa Madagascar 40 wamekuwa wakipewa ufadhili wa masomo kila mwaka katika vyuo vikuu nchini Urusi.
Pia, kupitia ushirikiano huo, Madagascar imekuwa ikinufaika katika sekta za nishati na vyakula na utamaduni. Mathalan, hivi karibuni, Urusi iliipatia Madagascar tani 80 za mafuta ya alizeti.
Wakati huo huo, Urusi inatekeleza mradi wenye thaamani ya Dola milioni nne, ambao utaimarisha upatikaji wa maji na nishati nchini katika maeneo ya Kusini mwa Madagascar.
Hata hivyo, swali ni je; ni uhusiano wenye afya kwa Madagascar? Ni kwa namna gani Madagascar inanufaika na misaada hiyo pasi na ‘kuibiwa’ rasilimali zake?
Wakati fulani, raia wa Madagascar walieleza wasiwasi wao juu ya kampuni ya madini ya Urusi, Ferrum Mining, kwamba inachota vya kutosha rasilimali hizo nchini kwao.


