LONDON, Uingereza
ARSENAL watakuwa ugenini nchini Hispania kuwakabili Atletico Madrid katika mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utakaochezwa kesho Aprili 29, 2026.
Baada ya mechi hiyo, timu hizo zitakutana tena wiki moja baadaye kwa nusu fainali ya pili itakayoamua nafasi ya kwenda fainali.
Atletico ina kumbukumbu mbaya ya kufungwa mabao 4-0 ilipokutana na Arsenal msimu huu wa Ligi ya Mabingwa.
Pia, vigogo hao wa mjini Madrid wameshinda mara mbili pekee katika mechi 12 walizocheza hivi karibuni dhidi ya timu za Uingereza. Wamefungwa nane na sare mbili.
Lakini, Atletico imezitoa timu za Uingereza mara zote tatu ilizokutana nazo hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Ulaya (Ligi ya Mabingwa na Ligi ya Europa), ikizifunga Liverpool (2009-10), Chelsea (2013-14) na Arsenal (2017-18)
Washika Bunduki walifika hatua hii baada ya kuitoa Sporting Lisbon kwa kichapo cha jumla ya bao 1-0, wakati Atletico iliwaondosha wenzao wa La Liga, Barcelona (3-2).
Kwa upande mwingine, Arsenal watashuka dimbani wakiwa na ‘mzuka’ baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Newcastle United.
Simeone ameizungumzia mechi yao dhidi ya Arsenal, akisema: “… Tunajua ubora na udhaifu wetu. Tunajiamini katika kile tunachofanya. Tuko tayari na tunakwenda kutimiza kile tulichokipambania kwa miaka mingi.”
Wakati Atletico wakiwa wamefunga mabao 34 msimu huu wa michuano hiyo, Arsenal wanajivunia safu ya ulinzi, ambayo imeruhusu matano pekee katika mechi 12.
Kwa upande wake, nyota wa Arsenal, Gabriel Martinelli, amesema: “Tunajiamini, tunajua ubora tulionao. Tuliwafunga katika mechi iliyopita lakini huenda hii ikawa tofauti.”
Vikosi: Atletitico – Oblak, Molina, Pubill, Le Normand, Ruggeri, Simeone, Llorente, Koke, Alex Baena, Griezmann na Alvarez
Arsenal – Raya, White, Gabriel, Saliba, Hincapie, Rice, Odegaard, Zubimendi, Saka, Gyokeres na Martinelli.


