16.3 C
New York

Ayatollah Ali Khamenei; Maisha, mamlaka na migogoro ya Iran

Published:

TEHRAN, Iran

HABARI kubwa kwa sasa katika siasa za ulimwengu ni hatua ya Marekani na Israel kuishambulia kwa mabomu nchi ya Iran.

Kubwa zaidi, ni mashambulizi hayo kumuua kiongozi wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei. Aliyetangaza kifo chake ni Rais wa Marekani, Donald Trump.

Awali, taarifa hiyo ni kama ilipuuzwa n kuonekana propaganda, hadi pale televisheni ya Taifa ya Iran ilipotangaza kifo cha Ali Khamenei.

Ali Khamenei aliyefariki akiwa na umri wa miaka 86, ni miongoni mwa viongozi waliomudu muda mrefu madarakani, akiwa ameiongoza Iran kwa miaka zaidi ya 30.

Ikimaanisha, ni kiongozi kuiongoza Iran tangu Taifa hilo lilipofanya mapinduzi ya Kiislam mwaka 1979.

Kwa mujibu wa Katiba ya Iran, Ali Khamenei alikuwa ndiye kiongozi wa Serikali na amiri jeshi mkuu, ingawa rais anakuwepo.

Wachambuzi wa siasa hawamtaji Ali Khamenei kuwa ni dikteta, bali kiongozi aliyesimamia na kupigania masilahi ya Iran.

Hata hivyo, bado kwa baadhi ya wachambuzi wanamtafsiri kuwa ni kiongozi aliyejilimbikizia mamlaka, ikiwamo kuwa na nafasi nyingi za uteuzi serikalini.

Ndani ya nchi, alijizolea ushawishi mkubwa, ikiwa ni pamoja na picha zake kuuzwa madukani, hali iliyomfanya kuwazidi mvuto hata marais.

Vyombo vya habari viliripoti kila alichokifanya Ali Khamenei, hivyo marais kuonekana kama picha tu iliyowekwa kikatiba.

Ali Khamenei alizaiwa mwaka 1939 mjini Mashhad, Kaskazini-Mashariki mwa Iran. Anatokea familia ya dini (Uislam), akiwa ni mtoto wa pili kati ya nane.

Baba yake alikuwa muumini mzuri wa Dhehebu la Shia, ambalo ndilo linaloongoza kwa wafuasi wengi nchini Iran.

Anatokea familia masikini

Akisimulia maisha yake, Ali  Khamenei aliwahi kusema: “Nilikuwa kwenye maisha magumu, kiasi kwamba ilikuwa ni kawaida kushinda na kulala ukiwa umekula mkate tu.”

Ali Khamenei ni mwanazuoni mkubwa wa Dini ya Uislam, ambapo alihitimu ngazi ya juu ya mafundisho ya Qur-an akiwa na umri wa miaka 11 tu.

Alipojitosa katika siasa, akawa mkosoaji mkubwa wa Shah, utawala wa kifalme uliokuwa ukiiongoza Iran wakati huo, ambao uliondoshwa kwa mapinduzi mwaka 1979.

Kwa miaka mingi, akawa ni mtu wa misukosuko kutoka kwa vyombo vya dola vya Shah, ikiwamo kujificha, kukamatwa na kusota gerezani mara kwa mara.

Baada ya mapinduzi, akateuliwa kuwa kiongozi wa Swala ya Ijumaa katika Mji Mkuu wa Tehran.

Mwaka 1989, Ali Khamenei aliteuliwa kuchukua nafasi ya aliyekuwa kiongozi wa Iran, Ayatollah Khomeini, ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 86

Kwanini anapingwa?

Wakosoaji wanasema alichokifanya ni kuachana na misingi aliyoachiwa na Khomeini na kutengeneza njia zake za utawala.

Kwa mujibu wao, ni pamoja na kupenyeza watu wake katika mifumo yote ya Serikali, licha ya kwamba dola ilikuwa chini ya rais.

Kwamba Ali Khamenei alikuwa na watu wake kwenye taasisi zote muhimu, zikiwamo bunge, mahakama, polisi na vyombo vya habari.

Kupitia vyombo hivyo, Ali Khamenei anakosolewa kwa matukio ya kukandamiza wapinzani wa kisiasa na wanaharakati waliojaribu kukosoa mienendo yake.

Mathalan, mwaka 1999 wanafunzi waliingia barabarani kupinga baadhi ya mambo lakini aliweza kuwanyamazisha kwa nguvu ya vyombo vya dola.

Kama hiyo haitoshi, maandamano ya mwaka 2019 yaliyotokana na raia kupinga kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta yalisababisha vifo vya raia.

Anakosolewa pia kwa mtazamo wake juu ya usawa wa kijinsia. Chini ya utawala wake, wanawake kupata elimu hakikuwa kipaumbele chake.

Kama itakumbukwa, mmoja ya wanaharakati wa haki za wanawake alihukumiwa kifungo cha miaka 38 gerezani na kucharazwa viboko 148.

Mwaka 2022, mwanamke mwenye umri wa miaka 22, Mahsa Amini, alifariki akiwa anashikiliwa na polisi, chanzo kikiwa ni kutokuvaa vizuri ‘hijab’ yake.

Maandamano ya kulaani kifo chake yalisababisha watu zaidi ya 500 kupoteza maisha, kwa mujibu wa ripoti ya wanaharakati wa haki za binadamu.

Uhusiano mbaya na Marekani

Baada ya shambulio la Septemba 11, 2021 nchini Marekani, Rais wa wakati huo, George W. Bush, aliinyoshea kidole Iran, kama alivyofanya kwa Iraq na Korea ya Kaskazini.

Marekani na mshirika wake, Israel, wanaitaja Iran kuwa ni mfadhili wa Kundi la kigaidi la Hezbollah lililoko Lebanon.

Pia, Marekani na Israel zimekuwa zikiishinikiza Iran kuachana na utengenezaji wa silaha za nyuklia.

Kwa madai yao yanayoungwa mkono pia na mataifa ya Magharibi, Iran ya Ali Khamenei inatengeneza kwa siri silaha hizo.

Katika kuipata wakati mgumu Iran, Marekani na washirika wake waliiwekea vikwazo vingine vya kiuchumi. Hii ilisabaisha Iran kukabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo uhaba wa ajira.

Mwaka 2025, vikosi vya jeshi la Israel viliishambulia Iran, vikilenga viongozi wa kijeshi na vinu vyake vya nyuklia.

Iran, kwa upande wake, nayo ilijibu mapigo kwa makombora yake kushambulia miji kadhaa ya Israel.

Ni hadi pale Marekani ilipoingilia kuisaidia Israel, ndipo Ali Khamenei alipoonesha kuzidiwa nguvu.

Januari, 2026, utawala wa Ali Khamenei ulikumbana na changamoto ya maandamano makubwa ya raia walioingia barabarani kuipinga Serikali.

Kwa madai kwamba imeshindwa kumaliza changamoto za kiuchumi zilizosababisha ugumu wa maisha mitaani.

Ni kutokana na maandamano hayo, ripoti za wanaharakati wa haki za binadamu zilidai kuwa watu 6,488 wamepoteza maisha na wengine 53,700 walishikiliwa na vyombo vya dola.

Wiki chache baadaye, Rais Trump alitoa tamko akisema wanajeshi wake hawatasita kuingia Iran endapo raia wataendelea ‘kuonewa’.

Akiwajibu, Ali Khamenei alisema: “Wamarekani wanapaswa kujua kwamba kama wataanzisha vita, safari hii itakuwa vita ya ukanda mzima (Mashariki ya Kati).”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img