19.8 C
New York

Wataalamu: Waandishi wasiishie kwenye uzinduzi wa miradi

Published:

Na Faraja Mulungu, Gazetini

MTAALAMU wa Uhifadhi na Maliasili nchini Tanzania, Allen Mgaza, ametoa wito kwa taasisi za Serikali, mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia kuwashirikisha waandishi wa habari katika hatua zote za utekelezaji wa miradi ya mazingira na uchumi wa buluu, akionya kuwa utaratibu wa kuwaita wanahabari miradi inapokamilika unadhoofisha uwezo wao wa kufuatilia na kuibua masuala muhimu kwa jamii.

Mgaza ambaye amebobea katika tasnia ya uhifadhi wa mazingira kwa zaidi ya miaka 15 sasa, amesema ushiriki wa waandishi unapaswa kuanzia hatua za kupanga miradi, kuingia mikataba, uwekezaji na utekelezaji wake hadi kukamilika, badala ya kuwahusisha zaidi wakati wa uzinduzi au kutangaza mafanikio.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Gazetini kando ya warsha ya Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira, wakiwamo waandishi wa habari, mkoani Morogoro, Mgaza amesema ushiriki wa mapema utawasaidia wanahabari kupata uelewa wa kina na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo.

“Tatizo kubwa katika miradi mingi ni kwamba waandishi wa habari wanahusishwa mwishoni, wakati tunataka waandike mafanikio, tumefanikisha hiki au tumezindua kile. Lakini mwanzoni, wakati wa kuingia mikataba au kupanga miradi, hawahusishwi,” amesema Mgaza.

Ameeleza kuwa endapo waandishi watashirikishwa tangu mwanzo, watapata nafasi ya kuelewa malengo ya miradi, kufuatilia utekelezaji wake na kuhakikisha taarifa sahihi zinafika kwa wananchi, huku wakikusanya maoni ya jamii ili kusaidia kuboresha utekelezaji wake.

Amesisitiza kuwa taasisi zinazotekeleza miradi ya mazingira zinapaswa kujenga utaratibu wa kufanya kazi na vyombo vya habari katika kila hatua, kwa kuwa ushiriki huo unaweza kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufuatiliaji wa ahadi zinazotolewa kwa jamii.

WWF, NGOs ziwezesha ziara za waandishi

Katika hatua nyingine, Mgaza ametoa wito kwa WWF, mashirika mengine ya kimataifa pamoja na asasi za kiraia na zisizo za kiserikali (CSOs na NGOs) kuweka nguvu katika kuwawezesha waandishi wa habari kutembelea maeneo yanayotekelezwa miradi ya mazingira, kujifunza na kupata taarifa kutoka kwenye vyanzo vya moja kwa moja.

Amesema kuna tofauti kubwa kati ya mwandishi kuripoti jambo alilosimuliwa na kuripoti baada ya kutembelea eneo husika, kuona kinachofanyika na kuzungumza na wahusika pamoja na jamii inayoathirika.

“Kuna tofauti ya kutoa taarifa uliyoisikia na taarifa ya kitu ambacho umejionea mwenyewe. Waandishi wanahitaji kupata nafasi ya kufanya ziara za kimafunzo, kujifunza na kuona shughuli zinazofanyika ili waweze kutoa taarifa sahihi zinazotokana na vyanzo vya uhakika,” amesema.

Amebainisha kuwa ziara hizo zinaweza kusaidia kuibua visa halisi na mifano ya mafanikio au changamoto (case studies) itakayoongeza ubora wa habari zinazohusu uchumi wa buluu, uchumi wa kijani na uwekezaji katika rasilimali za asili.

Awasisitiza waandishi kuelewa lugha ya mazingira

Mgaza amesema pamoja na kupata fursa za kutembelea maeneo ya miradi, waandishi wanapaswa kujenga uelewa wa dhana za kitaalamu zinazotumika katika sekta ya mazingira, ikiwamo uendelevu (sustainability), ili waweze kutoa taarifa sahihi na zinazoeleweka kwa wananchi.

Amesema baadhi ya dhana za mazingira na uhifadhi zina maelezo ya kitaalamu yanayohitaji mwandishi kuzifahamu kwa kina kabla ya kuziwasilisha kwa umma.

Ameongeza kuwa vyombo vya habari vina wajibu wa kuhakikisha taarifa zinazohusu mazingira na matumizi ya rasilimali zinafika kwa jamii kwa lugha rahisi, huku vikitoa nafasi kwa wananchi kueleza uzoefu, changamoto na maoni yao.

Kwa mujibu wa Mgaza, sauti za jamii (community voices) zinapaswa kuwa sehemu muhimu ya habari za mazingira kwa sababu wananchi wanaoishi katika maeneo yanayotekelezwa miradi au yanayotegemea rasilimali hizo wana uzoefu wa moja kwa moja unaoweza kusaidia kueleza hali halisi.

Amesisitiza kuwa kuunganisha uelewa wa kitaalamu, takwimu sahihi, ushahidi wa maeneo husika na maoni ya wananchi kutasaidia kuboresha uandishi wa habari za mazingira na kuhakikisha taarifa zinazotolewa zinachochea uendelevu na kuleta manufaa kwa jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Shoroba katika Taasisi ya Kuendeleza Shoroba za Kilimo Tanzania (AGCOT), John Banga, amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhamasisha wakulima kutumia mbinu za kilimo endelevu zinazolinda mazingira na kuongeza tija katika uzalishaji.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Shoroba katika Taasisi ya Kuendeleza Shoroba za Kilimo Tanzania (AGCOT), John Banga.

Banga amesema utoaji wa elimu kwa wakulima kuhusu mbinu hizo unaweza kusaidia kuboresha uzalishaji wa mazao huku ukihakikisha shughuli za kilimo haziathiri mazingira.

“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha kilimo endelevu kinachotunza mazingira, kutafuta masoko ya kisasa na kufikia azma ya taifa ya uchumi wa buluu na kijani,” amesema.

Ameeleza kuwa kilimo na mazingira vina uhusiano wa karibu, kwa kuwa uzalishaji wa kilimo unategemea kwa kiasi kikubwa hali ya hewa, upatikanaji wa mvua na viumbe mbalimbali vinavyosaidia kudumisha rutuba na afya ya udongo.

Related articles

Recent articles