Na mwandishi wetu, Gazetini
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, ametangaza kustaafu siasa na utumishi wa umma, akieleza kuwa atajiuzulu nafasi hiyo kuanzia Septemba 4, 2026.
Nchimbi amesema leo, Agosti 25, 2026, amemuandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumjulisha kuhusu uamuzi huo, kwa kuzingatia Ibara ya 50(2)(c) ikisomwa pamoja na Ibara ya 149(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema uamuzi huo umetokana na ahadi aliyompa Rais Samia Agosti 27, 2025, kwamba angemsadia yeye na Taifa kwa uwezo wake wote na kwa uaminifu, huku akiahidi kuwa endapo Rais angeona anahitaji Makamu mwingine wa Rais, angeachia nafasi hiyo.
“Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mhe. Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza ahadi yangu,” amesema Nchimbi.
Nchimbi amemshukuru Rais Samia pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa imani waliyoonyesha kwake na kumpa nafasi ya kulitumikia Taifa.
Aidha, amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote alichokuwa katika utumishi wa umma.
“Nawahakikishia kuwa nitaendelea kuwa raia mwema wa Tanzania,” amesema.
Uamuzi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi Septemba 4, 2026, siku ambayo Nchimbi amesema atastaafu nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


