26.3 C
New York

Idi Amin; Utata wa ‘birthday’, usaliti, na udikteta wake (7)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA sehemu iliyopita, tuliona Israel, Uingereza na hata India zikisitisha mahusiano ya kidiplomasia na Uganda ya Idi Amin, huku Libya, Umoja wa Kisoviet na Marekani zikibaki kuiunga mkono Serikali yake.

Unajiuliza kwanini Umoja wa Kisoviet ulimuona Idi Amin kama mtu muhimu kwao? Tunaanzia hapo. Endelea na makala haya yenye simulizi ya kusisimua.

Chini ya kiongozi wake, Leonid Brezhnev, Umoja wa Kisoviet uliichagua Uganda baada ya kuona nchi zingine mbili za Afrika Mashariki, kwa maana ya Tanzania na Kenya, zimeshawahiwa na China na mataifa ya Magharibi.

Umoja wa Kisoviet ukawa msambazaji mkubwa wa silaha za kivita, ikiitumia Uganda zana mbalimbali, zikiwamo bunduki, bastola na ndege za kijeshi.

Kufikia mwaka 1975, Uganda ikawa imeshapokea misaada ya kiuchumi yenye thamani ya Dola milioni 12 na ya kijeshi Dola milioni 48 kutoka Umoja wa Kisoviet.

Kupitia urafiki huo, pia ikielezwa kuwa Uganda ikisaidiwa na Ujerumani Magharibi, Idi Amin alipeleka maelfu ya wanajeshi wa Uganda katika nchi za Ulaya Mashariki, ikiwamo Czech, kwa ajili ya mafunzo.

Mwaka 1976, uhusiano wa Uganda na Israel uliingia doa jingine kubwa. Idi Amin aliruhusu ndege ya Ufaransa iliyokuwa imetekwa na Wapalestina wawili na Wajerumani wawili kutua katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe.

Ni ndege iliyokuwa ikitoka Tel Aviv, Israel, kuelekea Paris, Ufaransa. Ndege hiyo ilipotua Entebbe, watekaji hao waliungana na wenzao wengine watatu. Wakawa saba.

Katika tukio hilo, watekaji waliwaachia huru watu 156 waliokuwa si raia wa Israel. Hivyo, Waisrael 83 wakaendelea kushikiliwa.

Israel iliagiza makomandoo wao kuingia Uganda na hatimaye kuuteka Uwanja wa Ndege wa Entebbe, kabla ya kuokoa mateka wote, ingawa wengine walifariki katika mapigano yaliyotokea.

Aidha, tukio hilo lilishuhudia wanajeshi 45 wa Uganda wakipoteza maisha, pia taswira ya nchi hiyo ikiendelea kuwa mbaya kimataifa.

Historia iko wazi na inakumbusha kuwa ni tukio lililosababisha Serikali ya Uingereza kukerwa na hatimaye kufunga ubalozi wake nchini Uganda.

Wakati huo huo, zipo taarifa zinazodai kuwa varangati hilo liliibua sura ya uadui kati ya Uganda ya Idi Amin na Serikali ya Kenya ya wakati huo.

Inaelezwa kuwa Idi Amin alibaini na kukerwa na kitendo cha Kenya kuwasadia makomandoo wa Israel katika operesheni hiyo ya Entebbe.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, hasira za Idi Amin zilihamia kwa Wakenya waliokuwa wakiishi Uganda. Kwamba alitoa agizo la wengi wao kuuawa.

Usikose sehemu ya nane ya makala haya … Kama umepitwa na sehemu zilizopita, tembelea www.gazetini.co.tz

Related articles

Recent articles