Na mwandishi wetu, Gazetini
TULIISHIA wapi? Katika sehemu ya tano ya makala haya, tuliishia tukio la Juni 25, 1976, ambapo Baraza la Ulinzi la Uganda lilimtangaza Idi Amin kuwa Rais wa milele.
Katika sehemu ya leo, tunaangazia mahusiano ya Idi Amin na mataifa ya nje. Sera zake za kimataifa zilikuwa na sura ipi? Endelea …
Kwa kipindi chote cha mwaka wake wa kwanza madarakani, Idi Amin alipokea misaada muhimu ya kijeshi na fedha kutoka Uingereza na Israel iliyoungana naye kumpindua Obote.
Historia inaonesha kuwa Julai, 1971, alizitembelea nchi hizo kwa nyakati tofauti akiomba kusaidiwa vifaa vya kisasa vya kivita.
Kinyume cha matarajio yake, si Israel wala Uingereza, nchi zote zilikataa kwa madai kuwa Idi Amin alitakiwa kulipa fedha na si kupewa bure.
Hapo ndipo alipotafuta msaada kwingineko na kwenda nchini Libya katika ziara yake ya Februari, 1972, ambapo kiongozi wa wakati huo,
Muammar Gaddafi, alimpatia mkopo wa Dola milioni 25.
Kuanzia hapo, uhusiano wake na Israel na Uingereza ukayumba. Miezi michache baada ya msaada wa Libya, Idi Amin akawafurusha waliokuwa washauri wake wa kijeshi kutoka Israel.
Kama hiyo haitoshi, raia wa Israel 500 waliokuwa wakiishi Uganda nao walifukuzwa. Ni wakati huo, Uganda ilikataa pia kulipa Dola takribani milioni 18 ilizokuwa inadaiwa na Israel.
Hakuishia hapo. Idi Amin aliwatumia ujumbe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Kurt Waldheim, Waziri Mkuu wa Israel, Golda Meir, na kiongozi wa Palestina, Yasser Arafat.
Katika ujumbe wake huo, si tu alisema Israel siyo watu wenye manufaa kwa watu wengine duniani, bali pia alimsifu aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo, Adolf Hitler, na kuunga mkono uhalifu wowote dhidi ya Wayahudi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa upande mwingine, ukaribu wake na Gaddafi ukazidi kushamiri na kuota mizizi. Kama itakumbukwa, Gaddafi alisimamia na kumaliza mgogoro wa Uganda na Sudan.
Ni mgogoro ambao ulitokana na Idi Amin kuwaunga mkono waasi wa Anyanya katika vita dhidi ya Serikali yao nchini Sudan.
Katika jitihada zake, Gaddafi alifanikiwa kumshawishi Idi Amin kuacha na hatimaye mzozo huo ukafikia mwisho. Sehemu kubwa ya waasi hao walikuja kuajiriwa katika jeshi la Uganda.
Kwa upande mwingine, India nayo ilikata uhusiano wake wa kidiplomasia na Uganda, chanzo kikiwa ni Idi Amin kuwatimua raia wake nchini humo mwaka 1972.
Licha ya Uingereza nayo kusitisha urafiki, Uganda aliendelea kuwa chini ya mwamvuli wa Libya, Umoja wa Kisoviet na Marekani, ambayo hata hivyo haikufurahishwa na ujumbe wa Idi Amin kwa viongozi wa UN, Israel na Palestina.
Usikose sehemu ya saba ya makala haya … Kama umepitwa na sehemu zilizopita, tembelea www.gazetini.co.tz


