Na mwandishi wetu, Gazetini
HATIMAYE Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amewataja Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mstaafu, Dk. Phillip Mpango, na Waziri Mkuu Mstaafu, Kassim Majaliwa, katika kesi yake ya uhaini.
Lissu amewataja kama sehemu ya mashahidi wake baada ya kupatikana na kesi ya kujibu leo Agosti 21,2026, akiiomba mahakama kuwaita kwa ajili ya kumtetea katika shauri linalomkabili.
Kiongozi huyo amepatikana na kesi ya kujibu, ukiwa ni uamuzi uliosomwa na kiongozi wa jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru, akiwakilisha wenzake wawili; Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Aidha, Lissu alipopewa haki ya kujitetea au kukaa kimya, alisema atajitetea na kwamba ataita mashahidi na kutaja idadi ya mashahidi wake 11 ambao ameiomba mahakama itoe hati ya wito wa kufika mahakamani kwa ajili ya kumtetea.
Alisema idadi ya mashahidi hao inaweza kuongezeka na kwa kuanzia, ni pamoja na Rais Dkt. Samia, Dkt. Mpango na Majaliwa, Pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura.
Katika orodha yake ya mashahidi, pia Lissu aliwataja Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa na Ujasusi, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Chadema, Aman Golugwa; Makamu Mwenyekiti cha Chadema, John Heche, na Ofisa Habari wa Chadema, Brenda Rupia,
Wakati huo huo, Lissu pamoja na mashahidi hao, pia anao wengine, wakiwemo wanaharakati wa Uganda na Kenya, Agatha Atuhaile na Boniface Mwangi, Dkt. Willy Mutunga, Martha Kaluwa, na Mkurugenzi wa Jambo TV, John Marwa.
Ifahamike kuwa Lissu anashitakiwa kwa kosa la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code – PC) Rekenu ya mwaka 2023.


