19.6 C
New York

Idi Amin; Utata wa ‘birthday’, usaliti, na udikteta wake (5)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA sehemu iliyopita, aliyekuwa Waziri wa Afya katika uongozi wa Idi Amin, Henry Kyemba, alisimulia kupitia Kitabu chake cha ‘State of Blood: The Inside Story of Idi Amin’ cha mwaka 1977, kwamba ukatili wa kiongozi huyo ulitokana na kabila lake la Kkwa.

Kyemba akasema kama yalivyo makabila mengi ya kishujaa, watu wa jamii ya Kakwa walipendelea kutumia sadaka ya damu kwa maadui zao.

Akasema pia, kwamba katika moja ya mazungumzo yao, Idi Amin alisema aliwahi kula nyama ya binadamu. Sasa tuendelee na simulizi.

Eneo jingine ambalo wengi hawakupitia wa Idi Amin ni namna alivyokuwa na upendeleo kwa watu wa kabila lake (Wakakwa), Wasudan Kusini, na Wanubi.

Kufikia mwaka 1977, asilimia 60 ya majenerali wa jeshi na asilimia 75 ya Baraza la Mawaziri la Idi Amin walitoka katika jamii tatu hizo.

Ilishangaza wengi kwani jamii tatu hizo kwa pamoja ni asilimia 5 tu ya raia wa Uganda wakati huo. Asilimia 80 ya majenerali walikuwa Waislam, kama ilivyokuwa asilimia 87.5 kwa Baraza la Mawaziri.

Licha ya kuitwa mbaguzi, kwa Idi Amin ilikuwa na maana kubwa kuwapa nafasi watu wa jamii hizo na Dini yake. Ripoti zinaeleza kuwa ilimsaidia kukwepa majaribio nane ya kupinduliwa.

Tukirudi nyuma kidogo, wakati fulani Idi Amin alikosolewa kwa sera zake za kiuchumi, ambazo isivyo bahati ziliishia kunyanyasa wageni na hata Waganda wenye asili ya mataifa ya nje.

Tujikumbushe hotuba yake ya Agosti 4, 1972, ambapo alisema: “Tumedhamiria kuwafanya wananchi wa kawaida wa Uganda kuwa waamuzi na kuufurahia utajiri wa nchi yao.

“Sera yetu inalenga kuwapa wananchi wa Uganda uwezo wa kumiliki utajiri wa nchi yao, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii,” alisema.

Hata hivyo, kile alichokiita ‘vita vya kiuchumi’ kilishuhudia Serikali ikipokonya mali zilizokuwa zikimilikiwa kihalali na raia wa kigeni kutoka Asia na Ulaya.

Wageni ambao kwa wakati huo walikuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Uganda kutokana na kumiliki viwanda na biashara zenye mitaji mikubwa nchini humo.

Mbaya zaidi, hata Waganda 80,000 wenye asili ya India, ambao walizaliwa katika Taifa hilo la Afrika Mashariki, nao walipitiwa na upepo huo mbaya wa kupokonywa mali zao.

Kama hiyo haitoshi, Idi Amin alikuja na agizo la raia wote wa kigeni kutoka Asia (siyo wenye uraia wa Uganda) kuondoka na kurudi makwao, akidai kuwa walikuwa wakihujumu uchumi wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Idi Amin, alipata maelekezo hayo kutoka kwa Mungu, kwamba kuondosha wageni hao ni njia ya wananchi wa Uganda kustawi kiuchumi.

Baadaye, hata raia wa Uganda wenye asili ya Asia walikimbilia Uingereza, Australia, Afrika Kusini, Canada, India, Kenya, Pakistan, Sweden, Tanzania, na Marekani kutokana na mazingira magumu ya kuishi chini ya Idi Amin.

Mbaya zaidi, mali alizopokonya wageni aliwamilikisha watu wake wa karibu, ambao kimsingi hawakuwa na uzoefu. Hiyo ilisababisha biashara, kampuni na viwanda hivyo kufa na uchumi wa Uganda kuyumba kwa kiasi kikubwa.

Ikumbukwe, wafanyabishara kutoka Asia walikuwa wakichangia asilimia 90 ya mapato ya Serikali yatokanayo na kodi. Hivyo, kuondoka kwao kukaifanya Serikali ya Idi Amin kupoteza fedha nyingi.

Mwaka 1975, wakati huo hali ya uchumi ikiwa mbaya, aliyekuwa Waziri wa Fedha wa muda mrefu wa utawala wa Idi Amin, Emmanuel Bwayo Wakhweya, aliondoka na kukimbilia Uingereza.

Haikuchukua muda mrefu, aliyekuwa Waziri wa Afya, Henry Kyemba, naye alitimkia Uingereza, kabla ya kuandika kitabu chake cha ‘A State of Blood’ (Dola ya Damu) mwaka 1977.

Ilipofika Juni 25, 1976, udikteta wa Idi Amin ulichukua sura mpya baada ya Baraza la Ulinzi, ambalo yeye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wake, kumtangaza kuwa Rais wa milele wa Uganda.

Usikose sehemu ya sita ya makala haya … Kama ulipitwa na sehemu zilizopita, tembelea www.gazetini.co.tz

Related articles

Recent articles