NEW YORK, Marekani
MAPEMA wiki hii, Katibu Mkuu wa Marekani, Marco Rubio, aliijia juu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akiita kuwa ni yenye kuendeshwa kwa misingi ya rushwa na siasa.
Rubio alienda mbali zaidi na kutangaza hatua ya Marekani kumuwekea vikwazo Rais wa ICC raia wa Japan, Tomoko Akane, na mwanasheria mwandamizi wa Mahakama hiyo, Abdoulaye Seye wa Senegal.
Vikwazo vilivyohusisha pia kukamatwa kwa akaunti zao za benki zilizopo Marekani, pamoja na kukatishiwa huduma zote za kifedha nchini humo.
Taarifa ya ICC ikiijibu Marekani ilieleza: “Vikwazo hivi ni shambulizi dhidi ya uhuru wa taasisi ya Mahakama. Ni ukandamizaji wa utawala wa sheria.”
ICC imekuwa ikiwakamata na kuwafungulia mashitaka wahusika wa uhalifu dhidi ya binadamu, kivita na mauaji ya halaiki tangu mwaka 2002.
Mahakama hiyo ina Makao Makuu yake mjini The Hague, Uswis, kama ilivyo kwa Mahakama ya Kimataifa ya ICJ, ambayo iko chini ya Umoja wa Mataifa ikishughulika na migogoro ya nchi na nchi.
Tofauti na ICJ, ICC ina nchi wanachama 125 lakini si wote ni wanachama wa UN. Nchi 68 ziko ICC lakini hazimo ndani ya Umoja huo wa Mataifa.
Marekani, Urusi na China ni baadhi ya nchi kubwa ambazo hazina uanachama wa ICC. Zipo baadhi kutoa Asia na Afrika ya Kaskazini.
Sasa, kwa kuwa si wanachama wake, ICC haipaswi kujihusisha na masuala yote, hata kama yanahusisha uhalifu wa kivita, yanapotokea katika ardhi ya nchi hizo.
Lakini, ICC inaweza kufungua mashitaka dhidi ya nchi hizo endapo zitafanya uhalifu dhidi ya wanachama wake. Ni kama ilivyoamrisha kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kwa kuhusika katika uhalifu wa kivita katika nchi za Palestina na Ukraine.
Kwa upande mwingine, hii si mara ya kwanza kwa Marekani kuitunishia misuli ICC. Hivi karibuni, Rubio alitishia kuivunja Mahakama hiyo.
Pia, katika hotuba yake ya Julai, 2026, alitangaza hatua kadhaa ambazo Marekani inalenga kuziendea katika kampeni yake ya kuipinga ICC.
Hatua hizo ni pamoja na kuzuia vibali vya kuishi Marekani kwa wafanyakazi wote wa ICC na mashirika yote yanayofanya kazi na Mahakama hiyo.
Aidha, alisema nchi zote zinazopokea misaada ya Marekani zitakalia ‘kuti kavu’ endapo hazitoacha kuwa sehemu ya ICC. Je, ICC itahimili presha inayopewa na Marekani? Kwa baadhi ya wachambuzi wa siasa, inaweza isiwe rahisi.
Mathalan, baadhi ya kampuni za nje ya Marekani zinazofanya kazi na Mahakama hiyo zinaweza kuhofia kushirikiana na ICC zikihofia Marekani kuwekea vikwazo biashara zake.
Pia, kwa baadhi ya waendesha mashitaka wa ICC, huenda wakawa waoga kushughulika ipasavyo na masuala yanayoigusa Marekani wakihofia kuwekewa vikwazo.
Wakati huo huo, ICC bado inaungwa mkono na Umoja wa Ulaya (EU), ambayo iliitaka Mahakama hiyo kuchunguza Urusi kwa uamuzi wake wa kuivamia Ukraine.
Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, na mwenzake wa Baraza la Ulaya, Antonio Costa, kwa pamoja wanasema wako upande wa ICC katika mgogoro wake na Marekani.
Taarifa yao ya pamoja inasomeka: “ICC inasaidia upatikanaji wa haki kwa waathirika wa uhalifu katika maeneo mengi duniani. Ili kuifanya kazi hii, mahakimu na maofisa wanapaswa kutokuingiliwa, bila kupewa presha.”
Vilevile, ICC inaungwa mkono na Ujerumani, ambapo Waziri wake wa Mambo ya Nje, Johann Wadephul, alisema Mahakama hiyo inaifanya dunia kuwa salama zaidi.
Ufaransa kupitia kwa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ilieleza msimamo wake wa kuendelea kuiunga mkono ICC, pia ikilaani vikwazo vya Marekani kwa Mahakama hiyo.
Ni kama ilivyofanya Japan, ambayo ndiyo mchangiaji mkubwa wa fedha za uendeshaji wa Mahakama ya ICC. Akizungumzia vikwazo vya Marekani, Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Toshihiro Kitamura, ameeleza kushangazwa.


