Na mwandishi wetu, Gazetini
MAGEUZI ya Kidijitali ni kichocheo kingine muhimu cha maendeleo katika karne hii ya 21. Kwa maana nyingine, mageuzi ya kidijitali ni fursa nyingine ya kuharakisha maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.
Kwa kutumia teknolojia hizi kwa ufanisi, Tanzania itaongeza ushindani wake, itapanua wigo wa uchumi na huduma, kuboresha uwezo wa kufanya maamuzi, kuongeza huduma jumuishi za kifedha, kuendeleza matumizi ya huduma za kidigitali katika sekta mbalimbali, na kujenga uwezo wa kutumia tekonolojia mpya zitakazoibuka.
HATUA ZILIZOPIGWA
Tanzania imeshuhudia kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, upatikanaji wa intaneti yenye kasi na maendeleo ya serikali mtandao ambayo kwa kiasi kikubwa yameboresha utoaji wa huduma kwa jamii.
Huduma za kifedha kupitia simu za mkononi zimeleta mapinduzi kwenye sekta ya fedha, ambapo sehemu kubwa ya jamii imeweza kupata huduma za kibenki kupitia simu za mkononi na kusaidia watu wengi, hasa waishio vijijini.
Aidha, teknolojia za kidigitali zimeleta mabadiliko katika katika utoaji wa huduma za afya, elimu na kilimo, hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Wakati huo huo, kuibuka kwa vituo vya ubunifu na ongezeko la kampuni zinazochipukia zinazojihusisha na masuala ya teknolojia kunadhihirisha dhamira ya dhati ya nchi ya kuongeza matumizi ya teknolojia kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande mwingine, kumekuwepo na jitihada kubwa katika usimamizi wa taarifa ili kusaidia kufanya maamuzi na kuongeza ufanisi katika kufanya maamuzi.
Jitihada hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa mifumo ya kitaasisi ya usimamizi wa taarifa na uwekezaji katika miundombinu ya taarifa. Mfano wake ni kuanzishwa kwa vituo vya kuhifadhi na kulinda taarifa.
CHANGAMOTO
Maendeleo na mageuzi ya kidijitali nchini bado yanahitaji juhudi za ziada katika maeneo kadhaa – miundombinu, usalama wa kimtandao, gharama kubwa, uwezo mdogo wa watumiaji na vikwazo vya kisheria katika usambazaji na matumizi ya teknolojia.
Pia, kuna changamoto ya upatikanaji wa teknolojia kwa wananci, hasa maeneo ya vijijini, pamoja na uwekezaji na matumizi madogo ya teknolojia zinazoibuka, mathalan akili-unde (AI), ‘blockchain’ na ‘internet for things’
Aidha, kumekuwapo na wasiwasi kuhuku ukosefu wa uwiano kati ya maendeleo na maadili katika matumizi ya teknolojia mpya, hususan teknolojia za akili-unde.
Hivyo basi, ili kushughulikia changamoto hizi na kuhakikisha manufaa yake yanawafikia watu kwa kiwango kikubwa, itakuwa muhimu kuwkeza katika rasilimali watu, miundombinu na sera madhubuti zitakazosaidia kutumia teknolojia hizi kuharakisha maendeleo.
MATARAJIO
Mosi, kuwa na jamii yenye umahiri katika matumizi salama ya mitandao na teknolojia za kidijitali, na inayozingatia misingi bora na maadili kwa masilahi ya jamii na taifa.
Pili, Tanzania kuwa kitovu cha kikanda cha maendeleo ya teknolojia kinachohamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuendeleza ubunifu, kuchochea maendeleo na kuongeza ushindani wake katika soko la kimataifa.
Tatu, upatikanaji wa intaneti ya kasi na huduma za mawasiliano zenye zilizo na uhakika na za gharama nafuu kote nchini.
Nne, mfumo thabiti na jumuishi wa usimamizi wa takwimu na taarifa unaowezesha upatikanaji wa taarifa sahihi, za kuaminia na kwa wakati, huku taifa likidumisha mamlaka kamili ya udhibiti, kuhifadhi na kutumia taarifa hizo kwa mujibu wa sheria na masilahi ya kitaifa.
Tano, ongezeko la matumizi ya data kibiashara kwa lengo la kuongeza thamani yake kiuchumi na kuongeza ajira.
Sita, Taifa linaloongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini kwa uzalishaji wa programu za kompyuta na maudhui kidijitali, kwa matumizi ya soko la ndani na la kimataifa.
Saba, Taifa lililo mstari wa mbele katika matumizi matumizi ya teknolojia zinazoibuka, lenye nguvukazi yenye mtazamo wa kisasa ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.
Nane, Serikali mtandao inayotoa huduma bora, jumuishi, na zenye utashi kwa raia na biashara, kwa lengo la kuimarisha ubora wa huduma.


