24.7 C
New York

Nafasi ya Serikali za Mitaa katika utekelezaji wa Dira 2050

Published:

Na Hassan Mwasha

SERIKALI za Mitaa hapa nchini zimepitia mabadiliko mbalimbali kwa nyakati tofauti. Mathalan, mwaka 1962, Serikali ilifuta utawala wa kimila na kuanzisha Serikali za Mitaa, Mamlaka za Miji na Halmashauri za Wilaya.

Mwaka 1972, mfumo wa Serikali za Mitaa nao ulifutwa na kuanzishwa kwa ugatuzi wa madaraka lakini hatua hiyo kwa namna moja au nyingine ilisababisha kukosekana kwa ushiriki wa wananchi, hivyo kuathiri utoaji wa maamuzi sahihi.

Hivyo, Serikali ililazimika kurejesha mfumo wa Mamlaka za Miji mwaka 1978, na kisha Serikali za Mitaa mwaka 1982, lengo likiwa ni kuimarisha ushiriki wa wananchi na utoaji wa huduma.

Aidha, mabadiliko mengine makubwa yalishuhudiwa mwaka 1996, ambayo kwa kiasi kikubwa yalilenga kuimarisha ushiriki wa wananchi, uwajibikaji na kuongeza makusanyo ya fedha.

Tangu hapo, Serikali za Mitaa zimekuwa nyenzo muhimu na ya msingi katika kukuza ushirikishwaji, demokrasia na kuhakikisha sauti za jamii zinapenya na kupata nafasi ya kuchangia uchoraji ramani ya maendeleo ya Taifa.

Sambambana na hilo, uwepo wa Serikali za Mitaa unalenga kuhakikisha kuwa maamuzi, ukusanyaji na ugawaji wa rasilimali vinakwenda sambamba na mahitaji ya maeneo husika.

Aidha, umuhimu wa Serikali za Mitaa unaweza pia kuonekana dhahiri katika kujenga daraja kati ya wananchi na Serikali, pia kuhakikisha sera za kitaifa zinakwenda sambamba na mahitaji ya jamii.

Kama hiyo haitoshi, Serikali za Mitaa zinapokuwa imara hukuza mapato, kuimarisha mifumo ya kodi, kukuza ushiriki wa jamii, kuboresha utoaji wa huduma na kuhimiza uwajibikaji.

Hivyo basi, ili kufikia malengo makuu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050), ni ukweli ulio wazi kwamba panahitajika uwepo wa mamlaka za Serikali za Mitaa zilizo bora na zenye nguvu.

Matarajio katika utekelezaji wa Dira 2050 ni kuwa na mamlaka za Serikali za Mitaa zenye sura ya ujumuishi, zinazojitegemea, zinazowajibika kwa wananchi, na kuendeshwa bila vitendo vya rushwa.

Pia, ushirikiano wa wazi na wenye tija kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, unaohakikisha mgawanyo endelevu wa rasilimali na utoaji wa
huduma bora kwa ufanisi.

Vilevile, matarajio ni kuwa na Serikali za Mitaa zinazoimarisha mshikamano wa kijamii na kuweka mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji.

Wakati huo huo, Serikali za Mitaa zinazoimarisha ukuaji jumuishi na mgawanyo sawia wa rasilimali ili kukuza ustawi, kuongeza mshikamano na kasi ya utatuzi wa changamoto za kijamii.

Mwisho, utekelezaji na mafanikio ya Dira 2050 unategemea mfumo wa utumishi katika Serikali za Mitaa uliojikita kwenye misingi ya uadilifu.

Si tu uadilifu, bali pia utumishi unaozingatia sifa na uwezo katika kuajiri na upandishaji vyeo ili kuendeleza weledi na ufanisi katika utoaji wa huduma.

Related articles

Recent articles